Hatimaye, mshambuliaji hatari wa kimataifa wa Kamerun, Bryan Mbeumo (26), ametua rasmi katika uwanja wa Old Trafford baada ya Manchester United kukamilisha usajili wake kutoka klabu ya Brentford. Vigogo hao wa soka wametangaza rasmi kumsajili Mbeumo kupitia tovuti yao mnamo tarehe 21 Julai, wakimpa mkataba wa miaka mitano utakaomweka klabuni hapo hadi Juni 2030. Atavaa jezi namba 19.
Ingawa ada ya uhamisho haijawekwa wazi, shirika la habari la Uingereza, BBC, linaripoti kuwa Manchester United imetoa kiasi cha Pauni milioni 65 (sawa na takriban Shilingi bilioni 221 za Kitanzania). Kiasi hiki kinavunja rekodi ya mauzo ya wachezaji katika historia ya klabu ya Brentford.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Mbeumo hakuweza kuficha furaha yake, akisema, "Nilipogundua kuwa kuna fursa ya kuichezea Manchester United, sikusita. Sasa nipo hapa, kuichezea timu ambayo niliiota tangu nikiwa mtoto."
Usajili huu haukuwa rahisi kwa Manchester United. Inasemekana walijaribu mara tatu kumnasa nyota huyo. Ofa yao ya kwanza ya Pauni milioni 45 mwezi Juni ilikataliwa na Brentford. Walirudi tena na ofa ya pili ya Pauni milioni 55, ambayo pia iligongwa mwamba. Licha ya Mbeumo mwenyewe kukubaliana maslahi binafsi na Man United, klabu yake ya zamani ilisimama kidete hadi pale United walipoongeza dau na kufikia bei waliyoitaka.
Mbeumo, ambaye ni tegemeo katika timu ya taifa ya Kamerun, ni mshambuliaji wa kisasa anayeweza kucheza nafasi nyingi kwenye safu ya ushambuliaji, iwe pembeni au katikati. Anajulikana kwa kasi yake ya ajabu, uwezo wa kuwapita mabeki, ufundi wa mguu, pamoja na macho ya goli. Sifa hizi zilimfanya kocha mkuu wa Manchester United, Rúben Amorim, kummezea mate tangu msimu uliopita.
Baada ya kujiunga na Brentford mwaka 2019, Mbeumo alikuwa nguzo muhimu iliyosaidia timu hiyo kupanda daraja kuingia Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu wa 2020-2021, akifunga mabao 8 na kutoa asisti 11. Tangu wakati huo, amekuwa akifanya vizuri mfululizo, akihusika katika mabao zaidi ya kumi kwa misimu mitatu mfululizo. Msimu uliopita ulikuwa wa kilele kwake, akifunga mabao 20 na kutoa asisti 8 katika Ligi Kuu pekee.
Usajili wa Mbeumo unafuatia ule wa Matheus Cunha kutoka Wolverhampton Wanderers na beki kinda wa pembeni kutoka Paraguay, Diego Leon, kuonyesha kuwa Manchester United ipo siriazi katika kujenga upya kikosi chake cha ushindi.