Mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Nigeria, Victor Osimhen, anaripotiwa kulenga kujiunga na klabu ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika dirisha lijalo la usajili la majira ya joto. Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka chombo cha habari za michezo cha kimataifa, 'ESPN', ambacho kilieleza kuwa Osimhen anapanga uhamisho huo, au kujiunga na Juventus ya Italia, mara baada ya mkataba wake wa mkopo na klabu ya Uturuki, Galatasaray, kumalizika.
Osimhen amekuwa na safari ndefu kisoka, akipitia klabu kama Wolfsburg nchini Ujerumani na Lille nchini Ufaransa kabla ya kutua Napoli mwaka 2020. Ni akiwa na Napoli ndipo jina lake lilipoanza kuvuma kwa kasi. Katika msimu wake wa kwanza, alifunga mabao 10 katika mechi 30, na msimu uliofuata akafunga mabao 18 katika mechi 32.
Kilele cha mafanikio yake kilikuwa msimu wa 2022-23. Akifunga mabao 31 katika michezo 38, aliiongoza Napoli kutwaa ubingwa wa Serie A kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi. Mwisho wa msimu huo, alitwaa tuzo karibu zote binafsi nchini Italia, ikiwemo Mshambuliaji Bora wa Serie A, Mchezaji Bora wa Mwaka, na Mfungaji Bora.
Baada ya msimu huo wa kihistoria, Chelsea walijaribu kumsajili lakini hawakufanikiwa. Osimhen alibaki Napoli na msimu uliopita akafunga mabao 17 katika mechi 32. Katika dirisha la usajili lililopita la majira ya joto (2024), Chelsea walionyesha tena nia lakini wakashindwa kumpata. Wakati huo huo, klabu ya Al Ahli ya Saudi Arabia ilimshawishi kwa ofa nono ya mshahara. Ilionekana kana kwamba uhamisho huo ungekamilika, lakini dakika za mwisho Napoli walidaiwa kubadilisha dau la uhamisho na kutaka fedha zaidi, jambo lililosababisha mpango huo kuvunjika.
Taarifa kutoka Italia zinaeleza kuwa kuvunjika kwa uhamisho huo kulimkasirisha sana wakala wa Osimhen, ambaye anadaiwa kuwapigia simu Rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, na Mkurugenzi wa Michezo, Giovanni Manna, akitoa malalamiko makali. Tukio hilo lilisababisha uhusiano kati ya Osimhen na uongozi wa Napoli kuvunjika kabisa.
Matokeo yake, mwishoni mwa dirisha la usajili lililopita, Osimhen alijiunga na Galatasaray kwa mkopo. Akiwa Uturuki, ameendelea kuonyesha makali yake, akifunga mabao 28 na kutoa pasi za mabao 6 katika michezo 32 aliyocheza msimu huu. Inaonekana dhahiri kuwa hatarejea Napoli baada ya mkopo kuisha, bali atatafuta uhamisho wa kudumu.
'ESPN' imefafanua, "Osimhen anaonekana ataondoka katika dirisha la majira ya joto baada ya kumaliza msimu wake Galatasaray. Chanzo kimoja kilisema hakuna kipengele cha Galatasaray kumnunua moja kwa moja. Osimhen ameeleza kuwa anapendelea zaidi kuhamia Uingereza au Juventus."
Ripoti hiyo inaongeza kuwa klabu za Manchester United, Chelsea, na Arsenal zote zina nia ya kumsajili. Chelsea wana historia ya kumfuatilia, na Manchester United wamemweka kwenye orodha yao ya wachezaji wanaowataka.
Hata hivyo, suala la mshahara linaweza kuwa kikwazo. 'ESPN' inasema, "Inatarajiwa kuwa Osimhen atataka mshahara wa takriban Euro milioni 11 (kama Shilingi Bilioni 30.8 za Tanzania) kwa mwaka baada ya makato ya kodi. Vyanzo vinasema kuwa Manchester United wanajitahidi sana kupunguza gharama za mishahara katika dirisha hili la majira ya joto." Hii inaweza kufanya uhamisho wake kwenda Old Trafford kuwa mgumu zaidi.