Klabu ya Singida Black Stars, ambayo inajiandaa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake, imetangaza rasmi kuwa itatumia viwanja vya hapa jijini Dar es Salaam kwa mechi zake zote za nyumbani. Viwanja vilivyochaguliwa ni Uwanja wa Benjamin Mkapa na Azam Complex.
Uamuzi huo umefikiwa kutokana na viwanja hivyo viwili kuwa miongoni mwa viwanja vichache nchini vilivyokidhi vigezo na kupata ithibati kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya kuchezewa mechi za kimataifa.
Akithibitisha taarifa hiyo, Afisa Habari wa Klabu hiyo, Hussein Masanza, alisema tayari wamewasilisha taarifa rasmi kwa CAF kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu uamuzi wao huo.
"Ni kweli, tutatumia viwanja vya Dar es Salaam katika mashindano yetu ya kimataifa. Hivi ndivyo viwanja vyenye hadhi inayotakiwa na CAF. Tunawataarifu mashabiki wetu na Watanzania wote kuwa safari yetu ya kimataifa itaanzia hapa Dar es Salaam," alisema Masanza.
Aliongeza kuwa klabu inafanya maandalizi makubwa kuhakikisha inafanya vizuri na kuiwakilisha nchi kwa heshima katika michuano hiyo mikubwa. Singida Black Stars ilipata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho baada ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu uliopita.
Wawakilishi wengine wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho ni Azam FC, huku Simba na Yanga zikiiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.