Klabu ya Tanzania Prisons ipo katika kipindi muhimu cha maamuzi, huku bodi ya klabu hiyo ikitarajiwa kukutana kesho, Jumamosi, kupanga mustakabali wa timu, ikiwemo hatima ya Kocha Mkuu, Amani Josiah, aliyefanikiwa kuiokoa timu isishuke daraja. Wakati hayo yakijiri, jiji la Mbeya limepata chachu mpya kufuatia wapinzani wao wa jadi, Mbeya City, kurejea Ligi Kuu.
Akizungumza na wanahabari, Mtendaji Mkuu wa Prisons, John Matei, alithibitisha kuwa kikao hicho cha bodi kitafanya tathmini ya kina ya msimu uliopita na kujadili mustakabali wa benchi la ufundi. Kocha Josiah, aliyejiunga na timu hiyo Desemba mwaka jana akitokea Geita Gold, alimaliza mkataba wake baada ya kumaliza kazi ya kuibakisha timu ligi kuu kupitia mechi za mchujo ('play off').
"Mkataba wa kocha umekwisha, na bodi ndiyo itaamua baada ya tathmini kama tutaendelea naye au tutatafuta mwelekeo mwingine. Majibu yote yatapatikana baada ya kikao cha kesho," alisema Matei.
Wakati uongozi ukijipanga, wachezaji wote wamepewa mapumziko. Matei alieleza kuwa mchakato wa usajili utafuata baada ya maamuzi ya bodi, huku akifungua milango kwa mashabiki kutoa maoni yao kuhusu jinsi ya kuboresha kikosi kwa ajili ya msimu ujao. Alisema watafanya mazungumzo na wachezaji wanaowahitaji ambao mikataba yao imemalizika, huku wakipanga kusajili nyota wapya.
Katika hatua nyingine, Matei alielezea furaha yake kwa kurejea kwa Mbeya City Ligi Kuu, akisema ni jambo linalorudisha uhai na ushindani wa kweli katika soka la Mbeya.
"Tuliwamisi sana Mbeya City. Dabi ya Mbeya ni moja ya mechi kubwa na za kusisimua nchini. Mashabiki kote Tanzania walimisi upinzani huu. Ingawa uwanjani huwa ni vita, nje ya uwanja sisi ni ndugu. Kurejea kwao kutaongeza ladha kwenye ligi msimu ujao," alisema Matei kwa furaha.
Sasa macho na masikio ya wadau wa soka jijini Mbeya na kwingineko yanasubiri maamuzi ya kikao cha bodi ya Prisons, huku wakijiandaa kwa shamrashamra za dabi ya Jiji la Mbeya itakayotimua vumbi tena msimu wa 2025/2026.