Ndoto Yatimia: Vijana 22 Waliochaguliwa Kutoka Mitaani Kuivaa Yanga Kwenye Fainali ya Kombe la Safari Lager

sports | Thu Jul 10 2025


Ndoto Yatimia: Vijana 22 Waliochaguliwa Kutoka Mitaani Kuivaa Yanga Kwenye Fainali ya Kombe la Safari Lager

Kwa vijana 22 wenye vipaji vya soka kutoka mikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam, ndoto yao ya kucheza kwenye jukwaa kubwa la kitaifa imetimia. Baada ya mchujo mkali wa kusaka vipaji ulioendeshwa na Safari Lager, kikosi cha "Safari Champions" kimetangazwa rasmi na sasa kinajiandaa kwa pambano la kihistoria dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga SC.


Pambano hili la fainali ya Kombe la Safari Lager litapigwa Julai 26, mwaka huu, katika Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam. Mpango huu, ulioanzishwa kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vya vijana walio nje ya mfumo rasmi wa vilabu vya kitaalamu, umetoa fursa ya kipekee kwa wachezaji wenye umri kati ya miaka 18 na 24.


Mchakato wa uteuzi, uliosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ulihusisha makocha wabobezi na wawakilishi wa jamii ambao walizunguka katika mikoa tajwa kuwachagua wachezaji wenye uwezo wa kipekee. Zaidi ya hapo, mashabiki pia walipata fursa ya kushiriki kupitia upigaji kura kwenye tovuti maalum.


"Lengo letu halikuwa tu kuandaa mashindano," ilisema taarifa kutoka kwa waandaaji. "Tulitaka kubadilisha jinsi vipaji vinavyogunduliwa. Vijana hawa hawakusajiliwa, walionekana na jamii zao, makocha, na mashabiki. Hii ni timu iliyojengwa na Watanzania kwa ajili ya Watanzania."


Uongozi wa Yanga, kupitia kwa Meneja wake wa Habari na Mawasiliano, Ally Kamwe, umesema unajivunia kuwa sehemu ya tukio hili muhimu linalolenga kurudisha mpira wa miguu kwa watu.


"Huu si mchezo wa kawaida kwetu, tunaupokea kwa mikono miwili. Tunaamini katika nguvu ya soka katika kuunganisha vizazi na kutoa fursa. Ni heshima kwetu kuwa sehemu ya safari ya vijana hawa," alisema Kamwe.


Sasa, macho na masikio ya wadau wote wa soka nchini yataelekezwa kwenye Uwanja wa KMC, kushuhudia kama vipaji hivi vya mtaani vitaweza kuonyesha cheche zao mbele ya mojawapo ya klabu kubwa na kongwe barani Afrika.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.