Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Hemed 'Morocco' Suleiman, ameweka wazi silaha yake kuu atakayoitumia katika mchezo muhimu wa leo dhidi ya Niger: mfumo wa kisasa unaomtaka kila mchezaji, bila kujali anacheza nafasi gani, kuwa tishio langoni mwa adui na kuwa na uwezo wa kufunga bao.
Taifa Stars inashuka dimbani leo saa 10:00 jioni katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuikabili Niger katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026. Hata hivyo, matumaini ya Stars kutinga fainali hizo moja kwa moja yamefifia baada ya Morocco kujihakikishia uongozi wa Kundi E kwa alama 18, hivyo kibarua kilichobaki ni kupigania kumaliza katika nafasi ya pili na kuombea hesabu za kuwa "mshindwa bora" (best loser).
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Morocco alikiri waziwazi kuwa timu yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa umaliziaji makini, tatizo alilosema linaanzia ngazi ya klabu. "Ukweli ni kwamba tuna upungufu kwenye eneo la mbele; kupata mshambuliaji halisi namba tisa nchini kwa sasa ni changamoto. Tatizo hili halianzi timu ya taifa, linaanzia kwenye klabu zetu," alisema kocha huyo.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, amebuni mfumo mbadala. "Soka la kisasa limerahisisha mifumo, mchezaji yeyote anaweza kufunga. Tumejaribu kuutumia mfumo huu na tumeona mafanikio kidogo hata mabeki wameanza kufunga. Hii ndiyo silaha tutakayoitumia kuwamaliza Niger," aliongeza Morocco.
Pamoja na matumaini ya kushinda, hesabu za kufuzu kupitia nafasi ya pili bado ni ngumu. Stars inahitaji kushinda mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Niger leo na baadaye Zambia ili kufikisha alama 16. Hata hivyo, uwezekano wa kuwa "mshindwa bora" ni mdogo, kwani timu nyingi zinazoshika nafasi ya pili katika makundi mengine tayari zina alama nyingi zaidi, huku zikiwa zimesaliwa na mechi kadhaa mkononi.
Stars inatoka kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Congo siku tatu zilizopita, na sasa macho na masikio ya Watanzania yanaelekezwa Zanzibar kuona kama mbinu hii mpya ya "kila mtu ni mfungaji" itaweza kuipa timu ushindi muhimu.