Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kimeondoka nchini alfajiri ya leo kuelekea Congo Brazzaville kikiwa na dhamira moja tu: kupata ushindi na alama tatu muhimu katika mchezo wao wa Kundi E kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026. Kocha Mkuu, Hemed 'Morocco' Suleiman, amesisitiza kuwa huu ni mchezo wa "kufa au kupona" na hakuna matokeo mengine wanayoyafikiria zaidi ya ushindi.
Stars itashuka dimbani Septemba 9, katika mchezo wake wa sita wa kundi hilo, huku ikijua fika kuwa ushindi ugenini ni muhimu ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea na ndoto za kihistoria za kushiriki Kombe la Dunia. "Hatuna chaguo lingine. Kama tunataka kuweka hai matumaini yetu, ni lazima tushinde mchezo huu. Tunaenda kupambana kwa ajili ya alama tatu, hilo ndilo jambo la msingi," alisema Kocha Morocco kabla ya timu kuondoka.
Kocha huyo ameeleza kuwa ana imani na kikosi chake, akisema wachezaji wengi wa ndani bado wana "moto" kufuatia kiwango kizuri walichoonesha kwenye michuano ya CHAN iliyomalizika hivi karibuni. Ili kuongeza nguvu, kikosi hicho kimeimarishwa na wachezaji wanne wa kulipwa wanaocheza nje ya nchi: nahodha Mbwana Samatta (Le Havre AC, Ufaransa), Simon Msuva (Al Talaba SC, Iraq), Dismas Novatus (Goztepe FC, Uturuki), na Charles M'mombwa (Floriana FC, Malta), ambao uzoefu wao unatarajiwa kuwa nguzo muhimu katika mchezo huo mgumu wa ugenini.
Kwa sasa, Taifa Stars inashika nafasi ya pili kwenye Kundi E ikiwa na alama tisa, nyuma ya vinara Morocco wenye alama 15 ambao wameshinda michezo yao yote mitano. Hali hii inafanya mchezo dhidi ya Congo kuwa wa lazima kushinda ili kujiimarisha katika nafasi ya pili.
Baada ya mtanange huo, Stars itarejea nyumbani kujiandaa na mchezo mwingine muhimu dhidi ya Niger, ambao utapigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.