Mgunda Awatoa Hofu Mashabiki wa Namungo, Aahidi Kubaki Ligi Kuu

sports | Tue Apr 01 2025


Mgunda Awatoa Hofu Mashabiki wa Namungo, Aahidi Kubaki Ligi Kuu

Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amewatoa hofu mashabiki wa soka mkoani Lindi, akisema timu hiyo haitoshuka daraja. Badala yake, watajitahidi kwa nguvu zote kuhakikisha wanabaki kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.


Akizungumzia maendeleo ya timu hiyo, Mgunda alikiri kuwa hali si nzuri kwa sasa, kwani timu haipo katika nafasi salama kwenye msimamo wa ligi. Hata hivyo, alisisitiza kuwa ataendelea kupambana na kuwahamasisha wachezaji wake kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha mashabiki wa Lindi wanaendelea kuiona timu yao kwenye Ligi Kuu msimu ujao.


Mgunda, ambaye alichukua timu katikati ya msimu kutoka kwa Mwinyi Zahera, ameiongoza Namungo kushinda michezo minne tu, kupata sare moja, na kupoteza michezo saba kati ya 16 aliyoiongoza.


"Ni kweli hatupo vizuri sana, lakini matatizo hayakimbiliwi, bali yanatatuliwa. Nimezungumza sana na wachezaji wangu, na naamini tutakuwa bora zaidi kwenye mechi saba zilizobaki. Tunakutana na timu zote ambazo pia zinahitaji matokeo mazuri, lakini naamini tutafanya vizuri," alisema Mgunda, ambaye alikuwa mshambuliaji mahiri wa Coastal Union zamani.


Aliongeza kuwa kwa kuwa ligi inaelekea mwishoni na wamesalia na michezo saba tu, watahakikisha wanafanya vizuri ili kufikia lengo la kuibakisha timu kwenye Ligi Kuu.


Namungo kwa sasa inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 23. Nafasi hii, ikiwa itaendelea kubaki hivyo, inaweza kuipelekea timu kushuka daraja au kucheza michezo ya mchujo ili kubaki Ligi Kuu.


Timu hiyo inatarajiwa kucheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mzunguko wa 23, dhidi ya Pamba Jiji kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.