Majaliwa Kuwa Mgeni Rasmi Tuzo za BMT 2024, Vipengele Vipya Vyatambulishwa

sports | Tue May 20 2025


Majaliwa Kuwa Mgeni Rasmi Tuzo za BMT 2024, Vipengele Vipya Vyatambulishwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa mwaka 2024, ambayo itafanyika Juni 1 mwaka huu katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam. Hafla hii itakuwa mara ya tatu kufanyika, kufuatia mafanikio makubwa ya tuzo za mwaka 2022 na 2023, ambazo zilivutia zaidi ya washiriki 700 kutoka sekta mbalimbali za michezo.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Profesa Mkumbukwa Mtambo, alieleza kuwa maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa, na mchakato mzima unatarajiwa kuendeshwa kwa weledi na ubora wa hali ya juu. Profesa Mtambo alisisitiza kuwa tuzo hizo zinalenga kutambua, kuthamini, na kuenzi mafanikio ya wanamichezo na timu zilizofanya vizuri mwaka 2024, na kwamba mwaka huu wameongeza vipengele viwili vipya ili kuifanya hafla hiyo kuwa ya kipekee.


Baadhi ya vipengele vinavyowaniwa ni pamoja na:

  1. Mwanamichezo Bora wa Kiume na wa Kike
  2. Mwanamichezo Bora Kijana (wa Kiume na wa Kike)
  3. Mwanamichezo Bora kwa Watu Wenye Ulemavu
  4. Timu Bora ya Taifa ya Mwaka (Wanaume na Wanawake)
  5. Timu Bora ya Klabu ya Mwaka
  6. Kocha Bora wa Mwaka (Kiume na Kike)
  7. Mwanamichezo Bora kutoka Mashuleni
  8. Mwamuzi Bora wa Mwaka
  9. Mwanahabari Bora wa Michezo
  10. Mwanamichezo Nguli wa Zamani
  11. Mchezaji Bora wa Chaguo la Watu



“Mwaka huu tumekuja tofauti. Tumeongeza thamani ya tuzo kwa kuwatambua wanamichezo nguli wa zamani pamoja na kuweka kipengele cha mchezaji bora wa chaguo la watu,” alisema Profesa Mtambo. Aliongeza kuwa kupitia kipengele hicho, wadau na wananchi watapata nafasi ya kupiga kura kumchagua mchezaji bora wanayemuona anastahili, hatua ambayo itaongeza ushiriki wa jamii katika kuthamini mafanikio ya wanamichezo nchini.


Aidha, kamati hiyo itashirikiana na vyama na mashirikisho ya michezo ya kitaifa katika mchakato wa kutambua na kuchagua washindi wa tuzo, kwa kuzingatia ushindani na mafanikio ya mwaka 2024 katika mashindano ya kitaifa na kimataifa. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa tuzo zinatolewa kwa wale wanaostahili na kuongeza uhalali wa tuzo hizo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.