Msimu wa 2024-2025 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) umefikia tamati kwa shangwe kubwa kwa mashabiki wa Liverpool, baada ya timu hiyo kuthibitisha ubingwa wake kufuatia ushindi mnono dhidi ya Tottenham Hotspur. Katika mchezo uliopigwa kwenye dimba lao la nyumbani, Anfield, majogoo hao wa jiji walionesha ubabe kwa kuichapa Spurs mabao 5-1 kwenye raundi ya 34 ya ligi hiyo pendwa duniani.
Ingawa walikuwa wa kwanza kuruhusu bao kupitia kwa Dominic Solanke dakika ya 12 tu, Liverpool walijibu mapigo kwa mtindo wa aina yake. Magoli kutoka kwa Luis Diaz, Alexis Mac Allister, Cody Gakpo, na nyota wao Mohamed Salah yalibadilisha upepo wa mchezo haraka. Goli la kujifunga la mchezaji wa Tottenham liliongeza karamu ya mabao na kuihakikishia Liverpool alama tatu muhimu zilizoambatana na taji la ubingwa.
Ushindi huu uliwafikisha Liverpool kwenye alama 82, wakiwaacha washindani wao wa karibu, Arsenal, kwa tofauti ya alama 15 (Arsenal wakiwa na alama 67). Huku zikiwa zimesalia mechi nne tu kabla ya msimu kufikia mwisho, hakuna timu inayoweza kuwafikia tena kileleni, hivyo kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa England.
Hili ni taji la 20 la ligi kuu katika historia ndefu ya Liverpool, likijumuisha mataji 18 waliyoshinda kabla ya ligi hiyo kubadilishwa jina na kuwa Premier League. Tangu kuanzishwa kwa EPL, hili ni taji lao la pili, wakitwaa la kwanza msimu wa 2019-2020, na sasa wanarejesha heshima hiyo baada ya miaka mitano. Mafanikio haya yanawaweka kwenye kundi moja na wapinzani wao wakubwa wa jadi, Manchester United, kama timu pekee zilizowahi kushinda taji la ligi kuu ya Uingereza mara 20. Inafurahisha kwa mashabiki wa Liverpool kuona timu yao ikifikia rekodi ya Mashetani Wekundu, ambao hawajashinda taji hilo tangu msimu wa 2012-2013.
Mafanikio haya yanakuwa matamu zaidi kwa kuwa yanakuja katika msimu wa kwanza wa kocha Arne Slot. Kocha huyu Mholanzi alichukua mikoba iliyoachwa na Jurgen Klopp aliyeondoka mwishoni mwa msimu uliopita. Slot, ambaye alitoka kuiongoza klabu maarufu ya Uholanzi, Feyenoord, alikuwa tayari amejijengea jina barani Ulaya kama kocha mwenye mbinu za kisasa na uwezo mkubwa, akishinda ligi ya Uholanzi (Eredivisie) msimu wa 2022-2023 na kombe la ligi msimu wa 2023-2024. Ubingwa huu unathibitisha kuwa uamuzi wa Liverpool kumwajiri ulikuwa sahihi.
Slot amefanikiwa kuijenga Liverpool imara zaidi kwa kuendeleza mfumo wa kushambulia kwa kasi (pressing) ulioasisiwa na Klopp, lakini akiongeza umakini zaidi kwenye pasi fupi fupi na umiliki wa mpira ili kutengeneza mashambulizi. Uongozi wake wa utulivu na umakini umeipa timu uthabiti mkubwa.
Cha kushangaza zaidi ni kwamba Liverpool ilitwaa ubingwa huu bila kufanya usajili mkubwa wa kutisha. Walitumia kiasi kidogo sana kwenye soko la usajili. Usajili wao mkubwa ulikuwa kipa Giorgi Mamardashvili kwa Euro milioni 30 (takriban TZS Bilioni 87), ambaye hata hivyo walimtoa kwa mkopo kwenda Valencia, na winga Federico Chiesa kwa Euro milioni 12 (takriban TZS Bilioni 35). Kwa kiasi kikubwa, walikabiliana na msimu bila nyongeza kubwa ya wachezaji, lakini wakafanikiwa kutwaa taji.
Ni kweli kwamba kudorora kwa timu kama Manchester United na Tottenham, pamoja na kuyumba kwa Manchester City, kuliwapa Liverpool faida fulani. Hata hivyo, uwezo wao wa kuidhibiti Arsenal katika mbio za ubingwa na kiwango chao thabiti msimu mzima kinadhihirisha uwezo mkubwa wa kocha Slot. Zaidi ya hayo, mchango wa nyota mkongwe Mohamed Salah ulikuwa wa kipekee, akifunga mabao 28 na kutoa pasi za mabao 18, takwimu za kuvutia zilizoisaidia timu pakubwa kutwaa ubingwa.