Timu ya taifa ya mchezo wa Kabbadi ya ufukweni imepangiwa kundi A katika mashindano yajayo ya Kombe la Dunia, ambapo itakutana na kibarua kigumu dhidi ya wenyeji Malaysia, pamoja na timu za Hungary na China. Mashindano hayo makubwa yanatarajiwa kuanza rasmi Septemba 23 na kumalizika Septemba 29 mwaka huu, yakifanyika katika fukwe za kuvutia za Port Dickson nchini Malaysia.
Akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya timu, Mwenyekiti wa Chama cha mchezo wa Kabbadi Tanzania (TSA), Abdalah Nyoni, amesema droo hiyo imeongeza ari kwa wachezaji na sasa wamejipanga kuhakikisha wanapeperusha bendera ya Tanzania ipasavyo. Alisema kuwa kwa sasa kikosi cha timu kinaendelea kujifua vikali katika viwanja vya Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam, ili kujiimarisha kabla ya kuingia kwenye ushindani mkali unaowasubiri.
"Lengo letu kuu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo tutakaocheza. Tunajua ushindani utakuwa mkubwa, hasa kutoka kwa wenyeji, lakini wachezaji wetu wana morali ya juu na wanaendelea na mazoezi kuhakikisha wanakwenda wakiwa fiti," alieleza Nyoni.
Katika kutimiza azma hiyo, mwenyekiti huyo alibainisha kuwa kambi rasmi ya timu itaingia Septemba 8 mwaka huu katika Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala (KIU), kilichopo Gongo la Mboto, Dar es Salaam. Hii itakuwa ni hatua ya mwisho ya kuwaweka wachezaji pamoja na kunoa makali yao kabla ya safari.
Timu inatarajiwa kuondoka nchini Septemba 23, siku ambayo mashindano yataanza. Kutokana na hilo, uongozi wa chama umetoa wito kwa wadau mbalimbali, makampuni, na Watanzania wazalendo kujitokeza kuisaidia timu, hasa katika kuwawezesha wachezaji na viongozi kupata fedha za matumizi binafsi (posho) watakapokuwa nchini Malaysia.