Mji wa Shinyanga, maarufu kama 'Mji wa Almasi na Dhahabu', mwishoni mwa wiki hii uliweka kando shughuli zake za kibiashara na kilimo na kugeuka uwanja wa mapambano ya kiurafiki, kufuatia kufanyika kwa mbio za kishindo za Shinyanga Polisi Jamii Marathon. Tukio hili la aina yake limefanyika leo, Novemba 30, 2025, katika viunga vya kihistoria vya Viwanja vya Sabasaba, likiacha alama ya umoja na uzalendo kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na Magharibi.
Mbio hizi hazikuishia kuwakutanisha wakazi wa Shinyanga pekee, bali zilivuta 'majembe' ya kukimbia kutoka maeneo jirani ya Tabora, Mbongwe, Kahama na Misungwi, wote wakiwa na ajenda moja: kukimbiza mwenge wa amani na kuimarisha afya. Washiriki walichuana vikali katika kategori za kilomita 5, 10 na ile ya 'kufa mtu' ya kilomita 21 (Nusu Marathon), huku shangwe na nderemo zikitawala kila mwanariadha alipogusa utepe wa ushindi.
Siasa na Michezo: Katambi Mwaga Nondo Mgeni rasmi katika tamasha hilo la afya alikuwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, ambaye pia anashikilia wadhifa mzito serikalini kama Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi. Akiwa amevalia mavazi ya kimichezo yayoashiria utayari, Katambi alitumia jukwaa hilo kutoa "dozi" ya uzalendo kwa mamia ya washiriki.
Mhe. Katambi alilimwagia sifa Jeshi la Polisi kwa ubunifu wa hali ya juu wa kutoka maofisini na kuja "kula sahani moja" na raia kupitia michezo. Alisisitiza kuwa dhana ya Polisi Jamii inapochanganywa na michezo, inazaa tunda la upendo na kuondoa hofu kati ya raia na askari wao.
"Ndugu zangu, michezo ni dawa, michezo ni tiba. Mlichokifanya Jeshi la Polisi kupitia Marathon hizi ni kupandikiza mbegu ya uzalendo ambayo itamea mioyoni mwa wananchi. Tunawaomba mbegu hii ijae amani ili tuendelee kuishi kwa utulivu kama walivyoasisi wazee wetu. Tusikubali mtu yeyote au kikundi cha watu wachache wachezee amani hii kwa maslahi yao binafsi," alisisitiza Katambi huku akishangiliwa.
Aidha, alimuhakikishia umma kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Jemedari Mkuu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuwa mdau namba moja wa michezo, kwani inatambua kuwa taifa lenye afya ndilo taifa linalozalisha mali.
RPC Magomi: "Shinyanga ni Shwari" Kwa upande wake, "Kamanda wa Anga" wa Mkoa wa Shinyanga, RPC Janeth Magomi, ambaye pia ni mlezi wa Polisi Jamii Fitness Center, alieleza kuwa lengo kuu la mbio hizo si kushindana tu, bali ni kujenga daraja la udugu.
RPC Magomi alibainisha kuwa siri ya Mkoa wa Shinyanga kuendelea kuwa shwari na salama inatokana na ushirikiano dhabiti uliopo kati ya jeshi hilo na wananchi. "Sisi Polisi tukikaa karibu na wananchi, uhalifu unapungua kwa kiasi kikubwa kwasababu mwananchi anakuwa huru kutoa taarifa. Hapa Shinyanga amani imetamalaki, watu wanafanya kazi zao bila hofu, na hii Marathon ni kielelezo cha mahusiano hayo mazuri," alisema Kamanda Magomi.
Zawadi na Ujumbe Mahususi Kama ilivyo ada ya mashindano, washindi waliofanya vizuri na kuwatoa jasho wenzao waliondoka na tabasamu baada ya kukabidhiwa zawadi za fedha taslimu na vyeti vya pongezi. Vilevile, wadau mbalimbali wa maendeleo waliofanikisha tukio hilo walitambuliwa kwa mchango wao.
Kauli mbiu iliyobeba uzito wa siku hiyo ilisema: "Kimbia kwa Afya, Imarisha Usalama wa Raia na Mali zao", ujumbe ambao unatarajiwa kuendelea kuishi vichwani mwa wakazi wa Shinyanga huku wakisubiri kwa hamu msimu ujao wa mbio hizo.