Kimewaka Anfield: Salah 'Amchana' Kocha Slot Live, Asema Uhusiano Wao Umekufa na Anafanywa Kafara

sports | Mon Dec 08 2025


Kimewaka Anfield: Salah 'Amchana' Kocha Slot Live, Asema Uhusiano Wao Umekufa na Anafanywa Kafara

Hali ya hewa ndani ya klabu ya Liverpool imechafuka vibaya na kufikia sehemu ambayo inaonekana haiwezi kurekebishika. Katika kile ambacho Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limetaja kama "Mahojiano ya Hatari Zaidi katika Historia ya Ligi Kuu ya England (EPL)," nyota wa klabu hiyo, Mohamed Salah, amevunja ukimya na kumshambulia waziwazi kocha wake, Arne Slot.


Mfalme huyo wa Misri, ambaye amekuwa icon ya Anfield kwa miaka mingi, amedai kuwa uhusiano wake na kocha huyo "umepasuka" na kwamba klabu inajaribu kumtumia kama "Kondoo wa Kafara" (Scapegoat) kwa matokeo mabovu wanayopata.


Chanzo cha Vurugu: Kusugua Benchi Elland Road


Mlipuko huu wa Salah umekuja mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Leeds United uliopigwa Jumamosi (Desemba 6) katika uwanja wa Elland Road, ambapo Liverpool iliambulia sare ya 3-3. Katika mchezo huo, Liverpool—ambayo kwa sasa imeporomoka hadi nafasi ya 9 ikiwa na ushindi mmoja tu katika mechi tano—ilimweka Salah benchi kwa dakika zote 90.


Hii ni mechi ya tatu mfululizo kwa Salah kuanzia benchi (mara ya mwisho kuanza ilikuwa Novemba 26 dhidi ya PSV), jambo ambalo halijawahi kumkuta katika maisha yake ya soka tangu atue Liverpool mwaka 2017.


Salah Atema Cheche: "Sihitaji Kupigania Namba Yangu"


Akizungumza na waandishi wa habari kwa hasira katika eneo la kuchanganyia (Mixed Zone) mara baada ya mechi, Salah alimwaga yote yaliyokuwa moyoni:


  1. Kuhusu Benchi: "Siwezi kuamini nimekaa benchi dakika 90. Hii ni mara ya kwanza katika maisha yangu ya soka kuwekwa benchi mechi tatu mfululizo. Nimesikitishwa sana."
  2. Kuhusu Kocha Slot: "Nilikuwa nikisema kuwa nina uhusiano mzuri na Arne Slot, lakini ghafla imekuwa kama vile hatuna uhusiano wowote. Uhusiano wetu umekufa."
  3. Kuhusu Kufukuzwa: "Sijui sababu, lakini nahisi kuna mtu hataki nibaki kwenye klabu hii. Wanajaribu kunitupia lawama zote mimi (Scapegoat). Hilo ni wazi."
  4. Kuhusu Heshima: "Sihitaji kupigania namba yangu. Hiyo namba niliipata kwa jasho na mafanikio niliyoyaleta hapa."


Namba Hazidanganyi: Salah ni Nani Anfield?


Salah, ambaye sasa ana miaka 33 (sawa na Son Heung-min), si mchezaji wa kawaida.


  1. Ni mfungaji wa 3 wa muda wote wa Liverpool (Mabao 250 katika mechi 420).
  2. Msimu uliopita (msimu wa kwanza wa Slot), Salah alihusika katika mabao 57 (Mabao 29).
  3. Hata hivyo, msimu huu amefunga mabao 5 tu na kutoa pasi 3 za mabao katika mechi 19, jambo linalotumiwa na wakosoaji kusema "kashuka kiwango."


BBC: "Hakuna Njia ya Kurudi Nyuma"


Wachambuzi wa BBC wanasema kauli hizi za Salah si za bahati mbaya, bali zinaonekana kupangwa ili kufikisha ujumbe mzito. Wanasema Salah amechoshwa na wachambuzi na wachezaji wa zamani wanaodai kuwa yeye ndiye chanzo cha Liverpool kufanya vibaya msimu huu, wakati ukweli ni kwamba hata asipocheza, timu bado inapata matokeo mabovu.

Vyanzo vya ndani vinasema Salah haridhishwi na mfumo mpya wa mbinu wa klabu na sera zao za usajili ambazo anaona hazimthamini.


Saudi Arabia Yanukia


Wakati Salah akijiandaa kuondoka Desemba 15 kwenda kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), mustakabali wake Liverpool unaonekana kuwa mashakani licha ya kuwa alisaini mkataba mpya wa miaka miwili miaka minne iliyopita.


Tetesi za nguvu zinasema klabu za Ligi Kuu ya Saudi Arabia zimekaa mkao wa kula. Klabu ya Al-Hilal, inayofundishwa na kocha Simone Inzaghi, inatajwa kuwa ndiyo yenye nafasi kubwa ya kumnyakua "Mfalme" huyo ili akamalize soka lake huko kwa heshima na pesa ndefu.


Je, huu ndio mwisho wa enzi ya Mohamed Salah ndani ya Anfield? Dalili zote zinaonyesha ndoa imevunjika.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.