Mshambuliaji matata wa Manchester City, Erling Haaland (25), amejikuta akitupiwa lawama nzito na kuitwa 'mwoga' badala ya 'jini lake la mabao', kufuatia kitendo chake cha kumwachia mchezaji mwenzake kupiga penalti muhimu wakati wa fainali ya Kombe la FA nchini Uingereza. City walipoteza fainali hiyo kwa kichapo cha 0-1 dhidi ya Crystal Palace.
Shirika la habari la Uingereza, BBC, mnamo tarehe 17 Mei 2025, liliripoti, "Haaland atajisikia vibaya kila anapouona Uwanja wa Wembley. Alipata fursa ya kumaliza ukame wake wa mabao hapo, lakini alimpa mpira Omar Marmoush. Na penalti ya Marmoush iliokolewa na Dean Henderson." Mechi hiyo ya fainali ya msimu wa 2024-2025 ilifanyika katika Uwanja wa Wembley jijini London, ambapo Manchester City, licha ya kupiga mashuti 23, walishindwa kuona lango la Palace na hivyo kuambulia patupu.
Matokeo haya yanamaanisha kuwa Manchester City wamekosa Kombe la FA kwa msimu wa pili mfululizo, wakimaliza kama washindi wa pili. Cha kusikitisha zaidi kwa mashabiki wao, huu ni msimu wa kwanza kwa City kumaliza bila taji lolote kubwa tangu msimu wa 2016-2017, yaani baada ya misimu minane. Hii pia ni mara ya pili tu katika historia yake yote ya ukocha kwa Pep Guardiola kumaliza msimu bila kunyanyua kombe.
Kwa upande mwingine, Crystal Palace waliandika historia mpya kwa kutwaa taji lao la kwanza kubwa tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1905. Kabla ya hapo, walikuwa wamewahi kushinda mataji ya Ligi Daraja la Kwanza (Championship) na Ligi Daraja la Pili (League One). Hii ni mara yao ya kwanza kabisa kushinda Kombe la FA katika historia ya miaka 164 ya michuano hiyo (ilianzishwa 1871). Ushindi huu pia unawapa Crystal Palace tiketi ya kushiriki michuano ya UEFA Europa League (UEL) kwa mara ya kwanza msimu ujao.
Kwa Manchester City, kipigo hiki ni chungu mno. Walitawala mchezo kwa muda mrefu na kushambulia lango la Palace mfululizo, lakini juhudi zao zote ziligonga mwamba mbele ya umahiri wa kipa Dean Henderson. Kibaya zaidi, walifungwa bao la mapema dakika ya 16 kupitia shambulizi la kushtukiza lililofungwa na Eberechi Eze, na wakashindwa kusawazisha.
Kukosa taji hili kunathibitisha msimu mbaya kwa Man City. Ushindi wao pekee ulikuwa ni wa Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu, taji ambalo wengi hawalichukulii kama taji kubwa. Katika Ligi Kuu, wanapambana kwa shida kuwania nafasi ya nne, walitolewa mapema katika raundi ya nne ya Kombe la Ligi, na katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) walitolewa na Real Madrid katika hatua ya mtoano ya timu 16 bora.
Lawama kubwa imemwangukia Haaland. Licha ya kucheza dakika zote 90 na kupiga mashuti matatu (moja tu likilenga lango), kitendo chake cha kumwachia Marmoush kupiga penalti kilionekana kama kosa kubwa. Haaland ndiye mpigaji mkuu wa penalti wa City, lakini hakuchukua jukumu hilo. Baada ya kuubusu mpira, alimkabidhi Marmoush, ambaye shuti lake lilisomwa na kuokolewa na kipa Henderson.
Tukio hili linaongeza rekodi mbaya ya Haaland katika Uwanja wa Wembley, ambapo sasa amecheza mechi sita bila kufunga bao. Zaidi ya hayo, ameshindwa kufunga katika fainali nane mfululizo, na hivyo kuzua ukosoaji mkubwa kuhusu uwezo wake wa kuhimili presha na kuwajibika.
Kocha Pep Guardiola alisema, "Kusema kweli, nilidhani Haaland angependa kupiga penalti ile. Bado sijazungumza naye moja kwa moja kuhusu hilo. Penalti huathiriwa na hisia za wachezaji wakati huo. Pengine wachezaji waliamua kuwa Marmoush angekuwa na uhakika zaidi."
Hata hivyo, wachambuzi na magwiji wa soka walikuwa na maoni makali zaidi. Wayne Rooney alisema, "Haaland ni mshambuliaji mzuri lakini hawezi kamwe kuwa Lionel Messi au Cristiano Ronaldo. Wachezaji hao wasingeweza kamwe kumwachia mtu mwingine kupiga penalti katika hali kama ile. Akili ya Haaland inaathiri moja kwa moja uchezaji wake. Pengine alihisi presha ya kupiga penalti Wembley."
Alan Shearer pia alikubaliana na Rooney, akiongeza, "Kama mshambuliaji wa zamani, kama mtu angeniambia nisipige penalti, ningekasirika. Visingizio kama kukosa penalti awali au kurejea kutoka majeruhi havikubaliki. Sikuamini nilipomwona Haaland anampa mchezaji mwingine mpira apige yeye."
Kimsingi, kitendo cha Haaland kutojitokeza kupiga penalti kilionekana kama kukwepa jukumu. Kipa wa Crystal Palace, Dean Henderson, naye alithibitisha hili akisema, "Nilidhani Haaland ndiye angepiga. Sikuwa na uhakika nijirushe upande gani dhidi yake. Lakini alimpa Marmoush. Nilijua Marmoush atapiga wapi. Nilijua nitaokoa." Hali hii imemfanya Haaland kushuka hadhi kutoka 'jini' hadi 'mwoga', na sasa macho yote yanasubiri kuona kama ataweza kubadilika katika fainali zijazo.