Wakati mwingine katika soka, 'kukatalika' kunaweza kuwa mafuta ya kuongeza kasi ya mafanikio. Hdivyo unavyoweza kuelezea sakata la mshambuliaji hatari wa JKT Tanzania, Peter Paul. Wakati Benchi la Ufundi la Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) likiwa limejichimbia nchini Misri likiwa na kikosi cha nyota 28 kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), huku nyumbani Peter Paul ameamua 'kuongea' uwanjani kwa takwimu ambazo haziwezi kupingika.
Mshambuliaji huyo, ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji walioenguliwa kwenye chujio la mwisho kutoka katika orodha ya awali ya nyota 53, amegeuka kuwa tishio namba moja katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Takwimu hazidanganyi; Peter Paul sasa ndiye kinara wa ufungaji ligini akiwa ameweka kambani mabao matano, lakini cha kushangaza zaidi ni uwezo wake wa kipekee wa kutumia kichwa.
Katika soka la kisasa, washambuliaji wenye uwezo wa kuruka na kuweka mpira kimiani kwa kichwa ni lulu adimu. Peter Paul amethibitisha kuwa yeye ni 'Waziri wa Anga' wa msimu huu. Kati ya mabao yake matano yaliyomweka kileleni mwa chati ya wafungaji, mabao matatu yote ameyafunga kwa kichwa. Hii inamfanya kuwa mchezaji pekee ligini mwenye idadi hiyo kubwa ya mabao ya vichwa, akiwaacha mbali washambuliaji wengine wenye majina makubwa kutoka klabu vigogo kama Simba, Yanga na Azam FC.
Umahiri huu wa Peter Paul, ambaye alitua JKT Tanzania akitokea Dodoma Jiji msimu uliopita, unatoa ujumbe mzito kwa makocha wa timu ya taifa. Inaonekana kana kwamba kila anaporuka hewani kuwania mpira, anataka kuthibitisha kuwa uamuzi wa kumuacha ulikuwa na walakini.
Uchambuzi wa takwimu za ligi unaonyesha kuwa sanaa ya ufungaji kwa kichwa bado ni changamoto kwa wachezaji wengi. Mpaka sasa, jumla ya mabao 17 pekee ndiyo yamefungwa kwa njia ya kichwa katika ligi nzima. Katika 'kapu' hilo la mabao 17, Peter Paul pekee anamiliki asilimia kubwa, huku mpinzani wake wa karibu akiwa ni Matheo Antony wa Mbeya City ambaye amefanikiwa kufunga mabao mawili kwa kichwa.
Orodha ya wanaofuatia inajumuisha mchanganyiko wa mabeki na viungo washambuliaji ambao kila mmoja amefunga bao moja la kichwa. Hawa ni pamoja na beki wa kimataifa wa Simba, Rushine De Reuck, Chamou Karaboue, na Wilson Nangu. Kwa upande wa mabingwa watetezi Yanga, wamo Lassane Koume na kiungo mkabaji Mudathir Yahaya.
Orodha hiyo pia inapambwa na nyota wa Azam FC, Nassor Saadun na 'Mtu Hatari' Feisal Salum 'Fei Toto'. Wengine walioingia kwenye orodha hiyo ya wafungaji wa bao moja la kichwa ni Oscar Mwajanga wa Tanzania Prisons, Haroub Mohamed wa Coastal Union, Andrew Simchimba wa Mtibwa Sugar, Mudrick Shehe wa Fountain Gate, na Jaffar Kibaya wa Mashujaa FC.
Kitendo cha Peter Paul kuongoza orodha hii wakati akiwa nje ya kikosi cha timu ya taifa kinazua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa soka. Je, Taifa Stars imeacha 'silaha' muhimu inayoweza kubadili matokeo pindi mipira ya juu inapotumika? Muda utasema, lakini kwa sasa, Peter Paul anaendelea kutawala anga la Ligi Kuu Bara, akiwaacha mabeki wakigonga vichwa jinsi ya kumzuia.