Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Mauritania, Ahmed Mokhtar Ahmed, ameielezea siku waliyoichapa Jamhuri ya Afrika ya Kati kama "usiku wa dhahabu," baada ya yeye kufunga bao pekee na la kihistoria lililoivunjia timu yake ukame wa mabao na kuiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali ya michuano ya CHAN. Bao hilo la dakika ya tisa lilikuwa la kwanza kwa Mauritania katika michuano hiyo inayoendelea nchini Tanzania, Kenya na Uganda.
Kabla ya mchezo huo wa Jumamosi iliyopita, Mauritania ilikuwa imeshuka dimbani mara mbili dhidi ya Madagascar na wenyeji Taifa Stars, lakini katika michezo yote miwili safu yao ya ushambuliaji ilishindwa kutikisa nyavu. Hali hiyo ilionekana kuwapa presha kubwa, lakini Mokhtar, ambaye alikuwa tegemeo kubwa wakati wa mechi za kufuzu, alibadilisha hadithi na kuwapa mashabiki wa nchi yake sababu ya kushangilia.
Ushindi huo wa bao 1-0 uliipandisha Mauritania hadi kufikisha pointi nne katika Kundi B, na kufufua matumaini yao ya kusonga mbele katika hatua ya mtoano. "Ninawapongeza wachezaji wenzangu na pia kocha baada ya ushindi huu muhimu. Sasa tumeshinda mechi yetu ya kwanza kwenye CHAN, na tutatazamia kutoa matokeo bora katika mechi yetu ijayo, Mungu akipenda," alisema Mokhtar, akionyesha unyenyekevu licha ya kuwa shujaa wa mchezo.
Bao la Mokhtar si tu liliwapa alama tatu muhimu, bali pia limewaweka katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B, nyuma ya vinara Taifa Stars. Hii ina maana kuwa sasa wanahitaji matokeo mazuri katika mchezo wao wa mwisho ili kujihakikishia nafasi katika hatua ya robo fainali, jambo ambalo lilionekana kuwa gumu kabla ya usiku huo wa dhahabu kwao.