Kinyang'anyiro cha kumpata mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo kimepamba moto rasmi, baada ya Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa, Abdul Nondo, kuchukua fomu na hivyo kuingia katika pambano la moja kwa moja na kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Zuberi Kabwe.
Nondo alikabidhiwa fomu hiyo leo, Julai 15, 2025, ikiwa ni siku ya mwisho ya zoezi hilo, na hivyo kuweka bayana dhamira yake ya kuwania ridhaa ya chama kumpeperusha bendera katika uchaguzi mkuu ujao. Huu ni mwaka wa pili kwa Nondo kujitosa kwenye kinyang'anyiro hiki dhidi ya Zitto.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Nondo alikumbushia pambano la kura za maoni la mwaka 2020, ambapo alishindwa na Zitto Kabwe, lakini akasisitiza kuwa dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Kigoma Mjini haijawahi kuyumba.
"Siyo mara yangu ya kwanza kuomba ridhaa hii. Mwaka 2020 kura hazikutosha, lakini siku zote nimebaki kuwa mwanachama na kiongozi mtiifu," alisema Nondo. "Nimerudi tena mwaka huu nikiwa na uwezo, nia, na ufahamu wa kina wa changamoto za wananchi wa Kigoma Mjini. Ninaamini nitapata ridhaa."
Licha ya ushindani huo, Nondo ameahidi kubaki kuwa mwanafamilia wa ACT-Wazalendo na atamuunga mkono mgombea yeyote atakayepitishwa na chama, ili kuhakikisha ushindi unarudi nyumbani.
"Jimbo la Kigoma Mjini siyo la majaribio wala la kutafutia umaarufu. Ni jimbo la watu waelevu wanaojua wanataka nini," alisisitiza. "Tumejipanga kuhakikisha tunafanya kampeni za nguvu, kulinda kura zetu, na kupambana na hujuma zote kutoka kwa dola na CCM ili turejeshe heshima ya mji wetu na sauti makini Bungeni."
Hatua ya Nondo inafanya kura za maoni za ACT-Wazalendo katika jimbo hilo kuwa moja ya chaguzi za ndani zitakazofuatiliwa kwa karibu zaidi nchini, ikimkutanisha kiongozi kijana mwenye shauku dhidi ya mwanasiasa mkongwe na mashuhuri.