Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, ameizindua rasmi Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, ambayo imekuwa ikisubiriwa tangu mwaka 2016. Bodi hiyo inalenga kusaidia waandishi wa habari kushughulikia changamoto zao za kitaaluma na migogoro inayowakabili kabla ya kufikishwa mahakamani.
Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 3, 2025, jijini Dar es Salaam, ukihusisha wawakilishi kutoka sekta mbalimbali za habari nchini. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kabudi alieleza kuwa bodi hii ni hatua muhimu katika kuimarisha weledi wa taaluma ya uandishi wa habari, kuchochea uwajibikaji, na kulinda haki za waandishi.
“Bodi hii itawapa waandishi wa habari fursa ya kusuluhisha matatizo yao kwa njia ya kitaalamu na ya haki, badala ya moja kwa moja kuyapeleka mahakamani,” alisema Prof. Kabudi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na wadau wa habari, waandishi wa habari, na wawakilishi wa taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta ya habari nchini. Uzinduzi wa bodi hii unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya habari, huku waandishi wakihimizwa kufuata maadili ya taaluma na kuzingatia uwajibikaji katika kazi zao.