Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amesema kuwa serikali inakopa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ambayo itakuwa na manufaa ya kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Alisisitiza kuwa faida za miradi hiyo zitaonekana kwa miaka mingi ijayo.
Amesema kuwa deni la taifa la shilingi trilioni 97 za Kitanzania halikutokana na mikopo iliyochukuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pekee, bali ni mkusanyiko wa madeni ya muda mrefu, yakiwemo yale yaliyoanza kuchukuliwa tangu enzi za Rais wa kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Wasira aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama na viongozi wa CCM Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, katika kikao cha ndani. Kikao hicho kilikuwa sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo, ambayo ililenga kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na kusikiliza kero za wananchi.
"Tunakopa ili kufanya jambo ambalo tutaishi nalo na faida zake kwa miaka mingi, kizazi hiki na hata kizazi kijacho. Na lile deni sio kwamba amekopa Rais Samia trilioni 97, sio kweli. Lile deni linaongezeka na madeni mengine ya zamani ambayo tulishakopa tangu enzi za Nyerere. Alichukua miaka 40 kuanza kulipa, nayo yamo katika hesabu," alisema Wasira.