Wakili Moses Ambindilwe ameibuka mshindi kwa kura zote zilizopigwa katika uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society – TLS) kanda ya Iringa. Alishinda nafasi ya Mwenyekiti bila kupingwa, akipata kura zote 45 zilizopigwa na wanachama.
Ushindi huu, ambao utamwezesha kuliongoza chama hicho kwa miaka mitatu, unatarajiwa kuleta nguvu mpya katika TLS kanda ya Iringa. Katika salamu zake za shukrani, Wakili Ambindilwe alisema, "Uhai wa TLS si tu kwamba umerudi, bali umerudi kwa nguvu kubwa. Mwitikio huu wa wanachama unatupa matumaini makubwa sisi viongozi."
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, kulikuwa na ushindani mkali ambapo Wakili Jessey Mwamgiga aliweza kuibuka mshindi kwa kupata kura 19. Aliwashinda Emmanuel Chengula aliyepata kura 16 na Vedasto Chonya aliyepata kura 10.
Uchaguzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa masuala ya haki jinai, wakiwemo maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mahakimu kutoka Mahakama za Mwanzo na Mahakama Kuu, pamoja na wawakilishi kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RCO).
Baada ya kutangazwa mshindi, Wakili Ambindilwe aliahidi kuendeleza mafanikio yaliyopatikana tayari, kama vile utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo. Pia aliahidi kuendeleza mfuko wa kijamii unaosaidia wanachama katika nyakati za furaha na huzuni, na kuimarisha ushirikiano kati ya wanachama wa TLS na wadau wote wa mahakama kupitia shughuli za kitaaluma na kijamii.
Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya "Hakuna Marekebisho, Hakuna Uchaguzi," Wakili Ambindilwe alisisitiza kuwa "Kwa mujibu wa sheria, ni Tume Huru ya Uchaguzi pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuzuia au kuahirisha uchaguzi. Wanaotaka kufanya hivyo wanajaribu kulifanya suala hili kuwa la kisiasa badala ya kisheria."
Makamu wa Rais wa TLS Taifa, Wakili Laetitia Ntagazwa, aliwahimiza mawakili wote kujiunga na TLS na kushiriki kikamilifu katika shughuli zake. Alieleza changamoto zinazowakabili wanasheria, akisema kuwa baadhi ya watendaji wa mahakama huwapuuza na wakati mwingine kuwavunjia heshima mbele ya wateja wao. "Kuna wakati hakimu au jaji anaweza kumtisha wakili mbele ya mteja wake. Hii haijengi uhusiano mzuri wa kuaminiana," alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Iringa, Bi. Beatrice Nsana, alisema kuwa kila mtu anapaswa kutimiza wajibu wake kwa nafasi yake ili kulitumikia taifa. Kamanda wa TAKUKURU Mkoa, Bwana Victor Swela, aliahidi ushirikiano katika kuharakisha uendeshaji wa kesi za jinai mahakamani ili haki iweze kupatikana kwa wakati.
Akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa alisisitiza kuwa TLS ni mdau muhimu sana katika mfumo wa utoaji haki na utawala bora nchini. "Mkutano huu ni muhimu kwa maendeleo ya TLS. Uchaguzi wenu unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa kanda hii na taifa kwa ujumla. Ninaamini kuwa mtakaowachagua hawatazingatia maslahi yao binafsi," alisisitiza Jaji huyo. Aliongeza kuwa uchaguzi huo unapaswa kuonesha mwanzo mpya ndani ya TLS Iringa, na aliwataka viongozi wapya kusimamia maadili, kutoa huduma kwa jamii, na kulinda maslahi ya wanasheria wote wa kanda hiyo.