Ufadhili wa Nje Wakauka, Maelfu ya NGOs Nchini Zayumba

politics | Fri Jul 04 2025


Ufadhili wa Nje Wakauka, Maelfu ya NGOs Nchini Zayumba

Mustakabali wa maelfu ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini Tanzania upo katika hali tete, kufuatia kusitishwa kwa ufadhili kutoka kwa washirika wengi wa kimataifa, hali iliyosababisha mashirika mengi kuyumba na kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa jamii.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Taifa (NaCoNGO), Jasper Makala, alisema changamoto hiyo imekuwa kubwa hasa kwa mashirika yaliyokuwa yakitegemea ufadhili kutoka nje, akitolea mfano kusitishwa kwa ufadhili kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).


"Mashirika mengi yamesajiliwa kwa kutegemea ufadhili wa nje. Ufadhili huo unapositishwa, mashirika mengi yanakwama na kushindwa kujiendesha," alisema Makala.


Hata hivyo, Msajili wa NGOs nchini, Vickness Mayao, alifafanua kuwa shirika kutofanya kazi kwa muda haina maana kuwa limeshindwa au ni la "mfukoni". Alisema kati ya mashirika 10,990 yaliyosajiliwa nchini, mengine hukwama kwa sababu maombi yao ya ufadhili wa miradi yamekataliwa.


"Shirika linaweza kuwa na mradi mzuri lakini likakosa fedha kwa wafadhili. Sisi kama wasajili tunawapa nafasi ya kujipanga upya badala ya kuwafuta mara moja," alieleza Mayao.


Kutokana na changamoto hiyo, NaCoNGO imeandaa kongamano kubwa la kitaifa litakalofanyika jijini Dodoma kuanzia Agosti 11 hadi 13 mwaka huu. Kongamano hilo litafanya tathmini ya mchango wa NGOs katika miaka mitano iliyopita na, muhimu zaidi, kujadili na kuweka mikakati mipya na endelevu ya kujiendesha.


Bwana Makala alibainisha kuwa serikali ililiona tatizo hili na kutoa agizo la kutengenezwa kwa mkakati endelevu utakaoyapa mashirika mbinu mbalimbali za kujiendesha bila kutegemea wafadhili wa nje pekee. "Kongamano hili litatupa muda wa kutosha kujadili kwa kina mikakati hiyo ya kuviendeleza na kuviimarisha vyombo vyetu ili viendelee kuhudumia jamii," alihitimisha.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.