Hali ya sintofahamu na manung'uniko yalitawala katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kilichofanyika hivi karibuni, tarehe 7 Mei, 2025. Chanzo kikuu cha mijadala mikali ilikuwa ni huduma isiyoridhisha ya nishati ya umeme inayotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo. Waheshimiwa madiwani walieleza kwa hisia kali jinsi wananchi wanavyoteseka kutokana na ukosefu wa umeme wa uhakika na kukatika mara kwa mara, huku baadhi ya maeneo yakiwa hayajawahi kuonja mwanga wa umeme tangu kuumbwa kwa dunia.
Hoja nzito ziliibuliwa wakati wa mjadala wa taarifa ya utendaji kazi iliyowasilishwa na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga. Madiwani, kwa kauli moja, walionyesha kutoridhishwa na utendaji wa shirika hilo, wakisema kuwa maboresho yanayofanywa hayaendani na mahitaji halisi ya wananchi. Walieleza kuwa hali hii inarudisha nyuma maendeleo na kuathiri shughuli za kila siku za kiuchumi na kijamii.
Akichangia kwa uchungu, Diwani wa Kata ya Mwamalili, Mheshimiwa James Matinde, alisema hana sababu hata moja ya kulipongeza TANESCO kwani katika kata yake nzima, hakuna hata kijiji kimoja kilichounganishiwa umeme. "Ni aibu kwa shirika kubwa kama TANESCO kushindwa kupeleka umeme hata katika kijiji kimoja tu cha kata yangu. Wananchi wanatuuliza sisi, na hatuna majibu ya kuwapa," alisema Matinde kwa masikitiko.
Naye Diwani wa Kata ya Chibe, Mheshimiwa John Kisandu, alielezea kero ya Mtaa wa Mwamapalala ambao umekuwa gizani kwa kipindi kirefu licha ya maombi kadhaa kuwasilishwa TANESCO. Alidai kuwa wamekuwa wakipigwa danadana na kupewa ahadi hewa zisizotekelezwa. "Kama TANESCO wanaona haiwezekani kupeleka umeme Mwamapalala, ni bora watuambie ukweli ili wananchi waendelee na matumizi yao ya vibatari na koroboi, kuliko kutupa matumaini yasiyo na tija," alisisitiza Kisandu.
Mjadala uliendelea kupamba moto huku Diwani wa Kizumbi, Mheshimiwa Rubeni Kitinya, akilalamikia ukosefu wa umeme katika maeneo muhimu ya huduma za jamii, akitolea mfano Zahanati ya Lyandu ambayo imekuwa ikifanya kazi bila umeme kwa muda mrefu, jambo linalohatarisha utoaji wa huduma bora za afya. Hata Diwani wa Viti Maalum, Mheshimiwa Pica Chogelo, hakuwa nyuma, akilalamikia tabia ya umeme kukatika mara kwa mara, hasa wakati ambapo mashabiki wa soka wanajiandaa kutazama mechi muhimu, jambo linalozua taharuki na hasara kwa wamiliki wa vizimba vya kuonyeshea mpira.
Hoja nyingine iliyoibua mjadala mkali ilitoka kwa Diwani wa Mwawaza, Mheshimiwa Juma Nkwambi. Alielezea wasiwasi wake kuhusu upotevu wa nguzo za umeme zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya mradi katika kijiji cha Ishoshandili. Alidai kuwa mradi huo ulitengewa nguzo 170 lakini zilizofika ni 75 tu, na kuhoji ziliko nguzo 95 zilizobaki, akihofia kuwa huenda zimeuzwa isivyo halali.
Akijibu hoja hizo nzito, Meneja mpya wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Seraphine Lyimo, alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi kwa haraka. Alionyesha kushtushwa na taarifa kuwa Kata ya Mwamalili haina umeme hata katika kijiji kimoja na kuahidi kutembelea maeneo yote yenye kero ili kujionea hali halisi. "Mimi ni mgeni hapa, lakini nawahakikishia kuwa tutashughulikia changamoto hizi. Pia, kuna habari njema kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameshasaini mradi mkubwa wa umeme unaofadhiliwa na wahisani, ambao utafika kila kona ya mkoa huu na kutatua tatizo hili kwa kiasi kikubwa," alieleza Mhandisi Lyimo, akiwataka madiwani kumpa ushirikiano.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mheshimiwa Elias Masumbuko, alihitimisha mjadala huo kwa kuwasihi madiwani kutoa ushirikiano wa dhati kwa meneja huyo wa TANESCO atakapoanza ziara zake za kikazi ili kuwezesha utatuzi wa haraka wa kero hizo za umeme zinazowakabili wananchi.