Serikali imetoa wito kwa Watanzania kubadili mtazamo na kuanza kuwekeza kwenye afya zao binafsi kwa kuweka akiba maalum kwa ajili ya matibabu, ikisisitiza kuwa huduma za kiafya zinagharimu fedha nyingi na haziwezi kuwa bure kwa asilimia mia moja. Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliyehimiza dhana ya uwajibikaji binafsi katika sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki maalum kwa wagonjwa wenye mahitaji ya faragha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Chalamila alifafanua kuwa gharama za uendeshaji wa hospitali, ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba pamoja na nishati kama umeme, hufanya iwe vigumu kwa huduma kutolewa bila malipo yoyote. "Haiwezekani mtu awe tayari kutumia fedha kwenye anasa na mambo mengine lakini anapofika kwenye suala la afya yake anategemea iwe bure kabisa. Ni lazima sote tuchangie ili kuboresha sekta hii," alisisitiza Chalamila.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa alieleza umuhimu wa sekta binafsi katika kusaidia serikali kutoa huduma za afya kwa mamilioni ya Watanzania. Alisema taasisi hizi zinafanya kazi kubwa ya kuokoa maisha na hivyo kuna haja ya kuwepo kwa mfumo wa kisheria utakaolinda uwekezaji wao. Alionya kuwa ipo hatari wawekezaji hao wakikata tamaa na kubadilisha matumizi ya majengo yao, jambo litakalosababisha pengo kubwa katika utoaji huduma. "Lazima tuwaunge mkono wenye nia thabiti kwa kuwa na sheria rasmi, ili tujihakikishie huduma endelevu na pengine kuwasaidia kupunguza gharama," aliongeza.
Ufunguzi wa kliniki hiyo mpya Mloganzila ni sehemu ya mkakati wa serikali kuboresha huduma za kibingwa nchini ili kuhudumia wagonjwa wanaohitaji faragha zaidi, viongozi, na hata wageni kutoka nchi jirani, na hivyo kupunguza idadi ya Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.
Akitoa takwimu, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk. Delilah Kimambo, alithibitisha uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma bobezi. Alisema tangu kuanzishwa kwa huduma hizo, takriban wagonjwa 180 wamepatiwa matibabu ya kupunguza uzito kwa njia ya puto, huku wengine 16 wakifanyiwa upasuaji mkubwa wa tumbo. Aidha, hospitali ya Mloganzila pekee huhudumia wagonjwa wa nje (OPD) kati ya 1,000 hadi 1,200 kila siku.