Serikali, kupitia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, imechukua hatua madhubuti kuingilia kati mgogoro sugu wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Ruvu Marwa, wilayani Same. Katika mkutano wake na wananchi, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo la siku 14 kwa Maafisa Ardhi wa mkoa na wilaya, kushirikiana na pande zote mbili, ili kupata suluhisho la kudumu la matumizi ya ekari 2,787 zinazogombaniwa.
Ili kuhakikisha utafutaji wa suluhu unaenda vizuri na kwa amani, Babu ameamuru kusitishwa mara moja kwa shughuli zote za kilimo na ufugaji katika eneo hilo kwa muda wa siku 14. Alizitaka pande zote kumchagua timu ya wawakilishi itakayoshirikiana na serikali kufikia muafaka wa haki na wa kudumu kwa manufaa ya wakazi wote wa Ruvu Marwa.
Mbali na kusuluhisha mgogoro huu, Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa Serikali itaungana na wataalam wa masuala ya ardhi na maji ili kutafuta njia bora za kudhibiti mafuriko yanayokumba eneo hilo mara kwa mara na kuharibu mashamba ya wakulima. Alibainisha kuwa Mkuu wa Wilaya alishatoa agizo la kugawa ekari 260 kwa wakulima waliokumbwa na mafuriko, lakini ugawaji huo ulizua utata baada ya kugawiwa ardhi zaidi ya ilivyoelekezwa, jambo lililochangia sintofahamu.
Katika mazungumzo yake, Mkuu wa Mkoa alitoa onyo kali kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, akimsihi kuacha upendeleo na kuongoza kwa haki bila kuegemea upande wowote, kwani wananchi wote walimchagua kwa lengo la kuwatumikia wote bila kubagua. Mkuu wa Mkoa alisisitiza kuwa Serikali iko upande wa haki na haitaegemea upande wowote, iwe ni wa wakulima au wafugaji.
Wakazi wa Ruvu Marwa, kupitia risala yao iliyosomwa na Penueli Mkomwa, walieleza kuwa maeneo yao yamekuwa yakikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara, hivyo kuwaachia hasara kubwa. Walishauri kuwa kuna eneo la wazi ambalo halishiki mafuriko, lakini lipo ndani ya pori tengefu. Kwa upande wao, wafugaji kupitia kwa kiongozi wao Isaya Lazaro, walisema kuwa eneo hilo la ekari 2,787 walikuwa wamepewa kihalali na serikali kwa ajili ya malisho. Walieleza kuwa kugawanywa kwa eneo hilo bila makubaliano kulichangia kuzuka kwa mgogoro. Wito wa RC Babu kwa wakazi hao ni kudumisha amani, utulivu, na umoja, bila kuruhusu tofauti za matumizi ya ardhi kuwagawanya.