Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, amegusa kero ya muda mrefu ya msongamano wa magari katika barabara kuu ya Morogoro, akiahidi kuwa serikali yake itatoa suluhu ya kudumu kwa kupanua barabara hiyo kuwa ya njia nne kuanzia Kibaha hadi Chalinze. Akizungumza na wananchi mkoani Pwani akiwa katika muendelezo wa kampeni zake, Mwalimu aliitaja barabara hiyo kama uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, akisema hali ya sasa ya foleni ndefu inakwamisha uzalishaji na kupoteza rasilimali muda.
Alifafanua kuwa barabara ya Kibaha-Chalinze ni lango kuu linalounganisha Jiji la Dar es Salaam na bandari yake na mikoa mingine yote ya Tanzania, pamoja na nchi jirani. Kutokana na umuhimu wake, barabara hiyo imeelemewa na idadi kubwa ya malori ya mizigo, mabasi ya abiria, na magari madogo, na kusababisha upotevu wa saa nyingi kwa wasafiri na wafanyabiashara.
"Haiwezekani barabara muhimu kama hii kwa uchumi wa nchi iwe chanzo cha kupoteza muda wa uzalishaji. Watu wanakaa kwenye foleni badala ya kuwa viwandani au mashambani. Mkitupa ridhaa, sisi kama CHAUMMA tutahakikisha tunajenga njia nne za lami kutoka Kibaha mpaka Chalinze ili kurahisisha mtiririko wa magari na kukuza uchumi," alisisitiza Mwalimu.
Aliongeza kuwa ahadi hiyo si ya kubahatisha, bali ni sehemu ya sera kuu ya chama chake inayotilia mkazo ujenzi wa miundombinu imara katika maeneo ya kimkakati ya uzalishaji mali. Alisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona eneo dogo kama hilo likiendelea kuwa kero kwa miaka mingi ilhali uwezo wa kulitatua upo.
Mgombea huyo aliendelea na kampeni zake katika maeneo mbalimbali ya Kibaha, akiendelea kunadi sera za chama chake zinazolenga kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa wananchi kupitia mipango inayotekelezeka na yenye tija kwa taifa.