Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuendeleza matendo mema waliyokuwa wakifanya wakati wa mwezi wa Ramadhani, ikiwa ni pamoja na kuendelea na ibada na kuiombea nchi amani, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika Baraza la Idi lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, tarehe 31 Machi 2025.
Aidha, aliwataka wenye mamlaka wanaosimamia sheria za usalama barabarani kuzitekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuepusha ajali ambazo zinaweza kuzuilika katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Idd El Fitri.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa wakati wa sikukuu, shughuli za usafiri wa vyombo vya moto huongezeka barabarani, hivyo mamlaka zina jukumu la kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara kwa kusimamia sheria kwa ukamilifu.
Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama wa watoto katika viwanja vya sikukuu ili wananchi waweze kusherehekea kwa furaha na amani, huku wakidhibiti vitendo vyote vya udhalilishaji na uvunjifu wa amani.
Vile vile, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuendeleza tabia ya kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali, kama vile watu wenye ulemavu, wajane, wazee, yatima na watu wanaoishi katika mazingira magumu, kwa kuwapa sadaka kwa kiwango kilichoonekana wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa upande mwingine, Rais Dk. Mwinyi aliwashukuru waumini wasio Waislamu kwa ushirikiano wao mkubwa waliouonyesha kwa Waislamu wakati wa mwezi wa Ramadhani, akisema kuwa ni mfano wa kuigwa wa uvumilivu miongoni mwa waumini wa madhehebu tofauti, jambo ambalo alisisitiza lidumishwe kwa manufaa ya nchi.