Kufuatia matukio ya hivi karibuni ambapo baadhi ya akaunti za mitandao ya kijamii ziliingiliwa na watu wasiohusika, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetangaza kuanza kwa mpango kabambe wa mafunzo maalum kwa Maofisa ulinzi wa taarifa binafsi kutoka taasisi zote za umma na binafsi. Mafunzo haya yanatarajiwa kuanza mwezi ujao na yanalenga kuwapa wataalamu hawa ujuzi na mbinu za kisasa za kukabiliana na tatizo la udukuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Mhandisi Stephen Wangwe, alieleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa na lengo la kuwapa Maofisa hao mbinu bora za kusimamia ulinzi wa taarifa katika maeneo yao ya kazi. Pia, watafundishwa wao na wale wote wanaosimamia mitandao ya taasisi jinsi ya kujikinga na kuepuka kuingiliwa kwenye akaunti zao muhimu.
Mhandisi Wangwe alisema kuwa mafunzo haya ni muhimu sana kwa kuongeza uelewa na ustawi wa haki ya faragha na usalama wa taarifa binafsi za wananchi. Aliongeza kuwa mpango huu utaiwezesha Tanzania kuingia rasmi katika ulimwengu wa kistaarabu kwa kuhakikisha kuwa taarifa za watu zinalindwa kwa kiwango cha juu.
"Tunaelekea katika ulimwengu ambapo tunahakikisha faragha za watu na usalama wa taarifa za kila mmoja vinalindwa kwa nguvu zote. Heshima zetu kama taifa inategemea sana jinsi ambavyo taarifa zetu zimehifadhiwa," alisisitiza Mhandisi Wangwe.
Akizungumzia matukio ya hivi karibuni ya udukuzi wa akaunti za taasisi mbalimbali, Mhandisi Wangwe alisema kuwa matukio hayo yanagusa moja kwa moja suala la ulinzi wa taarifa binafsi. Alifafanua kuwa udukuzi ni kosa la kimtandao ambapo wahalifu huchukua utambulisho ambao si wao na kuutumia kwa malengo yao. Mafunzo haya yatasaidia sana katika kuzuia matukio kama hayo yasitokee tena.