Akiendeleza kampeni zake zenye hamasa, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amewasilisha ujumbe mzito kwa wananchi, akiahidi kurejesha mamlaka ya nchi mikononi mwao endapo atachaguliwa. Akizungumza kwa hisia mbele ya umati wa wananchi, Othman alisisitiza kuwa chanzo cha mateso na changamoto zinazowakabili Wazanzibari ni kuongozwa na serikali ambayo haikuwahi kupata ridhaa yao halisi.
Alifafanua kuwa kiongozi asiyechaguliwa na wananchi hawezi kamwe kuwa na wajibu wa kuwatumikia kwa dhati. "Mnapata mateso makubwa katika nchi hii kwa sababu hamjawahi kupewa madaraka ya kweli. Kiongozi ambaye hajachaguliwa na ninyi hawezi kuwathamini wala kuwatumikia kwa moyo. Hiyo ndiyo sababu kuu ya shida zetu leo," alisema Othman huku akishangiliwa.
Katika kilele cha hotuba yake, Othman aliweka nadhiri mbele ya Mwenyezi Mungu na umma, akisema anataka Urais si kwa ajili ya heshima yake binafsi, bali kwa heshima na mustakabali wa Zanzibar. Aliwataka wananchi kufanya maamuzi ya kijasiri katika sanduku la kura.
"Ninasimama hapa leo kuahidi hadharani kwamba nitaurudisha Urais huu mikononi mwa wananchi wa Zanzibar, ili ninyi wenyewe muwe na sauti na maamuzi ndani ya nchi yenu," alitangaza Othman. "Nakuombeni kwa moyo wote, mmkatae kwa kura nyingi watawala waliopo, na mnichague mimi niwe mtumishi wenu wa kweli. Nchi hii si mali ya kikundi cha watu wachache – ni mali yenu nyote!"
Ujumbe wake umetafsiriwa kama mkakati wa kujenga hoja ya msingi kwamba utawala bora na maendeleo ya kweli vitawezekana tu pale wananchi watakapokuwa na mamlaka kamili ya kuchagua na kuwawajibisha viongozi wao.