Maelfu ya wananchi walifurika katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Bumbwini, Kaskazini B Unguja, wakionyesha kiu ya mabadiliko na kumsikiliza mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman. Viongozi wa chama hicho walitumia jukwaa hilo kueleza masikitiko yao juu ya namna urithi na historia adhimu ya Zanzibar inavyohatarishwa na uongozi mbovu, ufisadi, na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Akihutubia umati huo, mgombea urais Othman Masoud Othman, alisema kiongozi asiyepata madaraka kwa ridhaa halisi ya wananchi hawezi kamwe kuwatumikia kwa dhati. Alieleza jinsi alivyoshuhudia mateso ya wananchi katika ziara zake, ambapo kila kijiji alichofika, kilio kikuu kilikuwa ni ukosefu wa maji safi na salama kwa zaidi ya miaka 60. Alisema hali hii ni kielelezo cha wazi cha serikali isiyowajibika kwa watu wake.
"Inasikitisha kuona nchi ya wastaarabu kama Zanzibar, yenye sheria za kulinda hata wanyama, lakini binadamu wanadhalilishwa na kuteseka bila huruma. Kinachoendelea ni dhulma na ufisadi uliokithiri," alisema Othman kwa uchungu.
Alikumbusha tukio la uchaguzi wa mwaka 2020, ambapo alidai watu 21 walipoteza maisha mikononi mwa vyombo vya dola ili kulazimisha ushindi wa utawala uliopo. Alisema kitendo hicho ni fedheha na kielelezo cha utawala wa mabavu usiostahili kuongoza. "Watawala wa aina hii hawafai. Lazima tuwakatae kwa nguvu zote kupitia sanduku la kura ifikapo Oktoba 29," alisisitiza huku akishangiliwa.
Naye kiongozi mwandamizi wa chama hicho, Hassan Jani Masoud, alihoji ni kwa nini wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuogelea kwenye dimbwi la ufukara ilhali miradi mikubwa ya uwekezaji inaendelea kila kona. Alijibu kuwa tatizo kubwa ni ukosefu wa uadilifu, ambapo miradi hiyo imekuwa ikitumika kama njia ya viongozi kujinufaisha badala ya kuwasaidia wananchi. Alimtaja Othman Masoud kama kiongozi msafi, mwenye msimamo na maono ya kuijenga Zanzibar mpya itakayothamini utu na haki za watu wake. "Othman si kiongozi wa msimu mmoja, bali ni kiongozi wa kizazi anayepigania mustakabali wa taifa letu," alisema Jani.
Kwa pamoja, viongozi hao walituma ujumbe mzito kwa Wazanzibari, wakiwataka wasikubali tena kunyanyaswa na kuamka ili kudai haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na ustaarabu.