Kinyang'anyiro cha urais nchini kimezidi kupata kauli nzito, huku mgombea kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Bw. Doyo Hassan Doyo, akitangaza kuwa serikali yake haitasita kutumia adhabu ya kifo kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa katika miradi ya maendeleo.
Akizungumza na wanahabari leo, Septemba 1, 2025, katika ofisi za chama hicho zilizopo Tandika jijini Dar es Salaam, Bw. Doyo alisema kuwa rushwa, na hasa tabia ya viongozi "kugawana asilimia," ndio chanzo kikuu cha miradi mingi ya maendeleo kukwama na kutoleta tija kwa wananchi. Alisema, “Tatizo hili limeota mizizi na linarudisha nyuma maendeleo ya taifa. Serikali ya NLD haitavumilia wala kufumbia macho uozo huu. Tutatunga sheria kali, na miongoni mwa adhabu itakuwa ni kunyongwa.”
Bw. Doyo amekuwa mgombea wa pili katika uchaguzi huu kutangaza hadharani nia ya kutumia adhabu ya kifo kama suluhisho la tatizo la ufisadi, jambo linaloashiria mwelekeo mpya na mkali katika ahadi za kisiasa za mwaka huu.
Ili kufanikisha azma yake, aliahidi kuijengea uwezo na kuiimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na mamlaka nyingine za udhibiti. Lengo ni kuhakikisha taasisi hizo zinafanya kazi zake kwa uhuru na ufanisi ili kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania wote na si wachache.
Wakati huohuo, Bw. Doyo alitangaza kuwa uzinduzi rasmi wa kampeni za chama chake umepangwa kufanyika Septemba 4, 2025, jijini Tanga. Alieleza kuwa NLD imejiandaa kikamilifu kwa uchaguzi, ikiwa imesimamisha wagombea 100 wa nafasi ya Ubunge na wagombea 1,000 wa Udiwani kote nchini.
Alihitimisha kwa kuwaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kumuunga mkono, akiahidi kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii pindi atakapopewa ridhaa ya kuiongoza nchi.