Hatimaye, kilio cha muda mrefu cha upatikanaji wa majisafi na salama kwa maelfu ya wakazi wa Kata ya Saranga wilayani Ubungo, Dar es Salaam, kiko mbioni kufikia tamati. Hii inafuatia kuanza kwa mradi mkubwa wa maji wa King’ong’o unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), ambao unatarajiwa kuwa mkombozi kwa takriban watu 92,000.
Akifanya ziara ya kikazi kukagua hali ya huduma hiyo wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, alijionea mwenyewe maendeleo ya mradi huo ambao utahudumia mitaa ya Michungwani, King’ong’o na Kimara B. Bw. Msando aliipongeza DAWASA kwa kazi kubwa wanayoifanya, huku akisisitiza umuhimu wa mradi huo kukamilika kwa wakati na kwa viwango vya hali ya juu ili wananchi waanze kupata huduma hiyo muhimu haraka iwezekanavyo.
"Nawapongeza sana DAWASA, na ninaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya maji. Hata hivyo, natoa wito kwa wananchi wenzangu wa Ubungo, tujenge tabia ya kutunza na kuhifadhi maji. Hii itatusaidia sana pindi changamoto za kiufundi zinapotokea," alisema Msando.
Kwa upande wake, Mhandisi Modesta Mushi, akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, alimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa mradi huo unatekelezwa kwa weledi mkubwa na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2025, na hivyo kuondoa kabisa adha ya maji katika maeneo yaliyolengwa.
Katika ziara yake, Mkuu huyo wa Wilaya alitembelea pia mitaa ya Tarakea na Kavimbilwa katika eneo la Mbezi Makabe, ambapo alieleza kuridhishwa kwake na hali ya upatikanaji wa maji, akionyesha kuwa juhudi za serikali zinaendelea kuzaa matunda katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.