Katika hatua inayoashiria msimamo mkali dhidi ya siasa za mgawanyiko, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Emmanuel Nchimbi, amepiga marufuku kabisa matumizi ya wimbo unaolenga kudhalilisha na kuchochea uhasama dhidi ya vyama vya siasa vya upinzani nchini. Akitoa agizo hilo kwa wana CCM wote, Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa chama tawala kina jukumu la kuwa mfano bora katika kukuza upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, hasa katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Tamko hilo kali lilitolewa na Balozi Nchimbi alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Obwele, Mji wa Shirati, Wilaya ya Rorya. Hii ilikuwa Ijumaa, tarehe 25 Aprili 2025, ikiwa ni sehemu ya siku yake ya nne ya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Mara.
Kabla ya kutoa katazo hilo, Katibu Mkuu huyo aliwakumbusha wananchi kuhusu wimbo mashuhuri wa hamasa uliotumiwa na majeshi ya Tanzania wakati wa Vita vya Kagera dhidi ya utawala wa Nduli Idi Amin Dada wa Uganda. "Nadhani mnakumbuka ule wimbo... 'Idi Amin akifa, mimi siwezi kulia, nitamtupa Kagera, awe chakula cha mamba'...," alianza Balozi Nchimbi, kabla ya kuwaomba wasikilize wimbo mwingine aliokuwa nao.
Akitumia simu yake kucheza wimbo huo kupitia mfumo wa sauti wa mkutanoni, ulisikika wimbo wenye mahadhi yanayofanana na ule wa vita, lakini maneno yake yalikuwa yamebadilishwa na kuwekwa mashairi yanayolenga kubeza na kuchochea hisia hasi dhidi ya vyama vya upinzani nchini. Baada ya kuusikilizisha, Balozi Nchimbi alionyesha kutokubaliana nao vikali.
"Nachukua fursa hii kuendelea kusisitiza juu ya amani, umoja, na mshikamano wetu," alisema Balozi Nchimbi. "Mwaka huu tuna Uchaguzi Mkuu. Ni kipindi chenye vishawishi vingi. Ni muhimu sana, hasa kwa wanasiasa, kupima kauli zao. Iwe ni wa CCM au vyama vingine, ni lazima watoe kauli zinazojenga na kuimarisha utaifa wetu. Ni wajibu wetu kuulinda utaifa huu kwa gharama zote."
Aliongeza kwa msisitizo: "Maneno yaliyomo kwenye huu wimbo ni ya kujenga chuki, siyo upendo. Ninapiga marufuku wimbo huu kutumika popote na wanaCCM. Sisi kama CCM tuna dhamana kubwa katika taifa hili. Tunapaswa kuongoza kwa vitendo, kuwaunganisha watu, na siyo kuwa chanzo cha migogoro. CCM ndiyo mlezi wa demokrasia hapa nchini."
Zaidi ya kuwataka wanaCCM kuacha wimbo huo, Balozi Nchimbi alitoa rai pia kwa viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kujiepusha na lugha za uchochezi. "Sote, CCM na vyama vingine, tuepuke kauli za chuki, shari na vurugu. Hata tukisikia kiongozi wa upande mwingine anatoa kauli za hatari, badala ya kumjibu kwa chuki, ni vyema kutafuta njia za kuwasiliana na watu wake wa karibu, labda ndugu zake kule Singida, wamshauri kuwa mwelekeo huo si mzuri," alishauri kama njia ya kutuliza joto la kisiasa.
Katika mkutano huo huo, Balozi Nchimbi pia aligusia maendeleo ya miundombinu, akimuagiza Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdalla Ulega, kuzungumza na wananchi wa Rorya kwa njia ya simu na kuwahakikishia kuhusu utekelezaji wa mradi wa barabara ya lami ya Mika – Utegi – Shirati – Kirongwe (kilometa 56), ambao zabuni yake imeshatangazwa na ujenzi unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Aprili 2025.