Jiji la Dar es Salaam leo linatarajiwa kuwa kitovu cha siasa nchini, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikifanya uzinduzi wa kishindo wa kampeni zake za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mgombea urais kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan, na mgombea mwenza wake, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, wataongoza tukio hilo katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, wakiahidi kunadi Ilani na sera za chama kwa hoja na weledi.
Akizungumza na wanahabari, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi, alitamba kuwa kampeni za mwaka huu zitakuwa za kipekee na za kihistoria. Alisisitiza kuwa chama chake kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu, zitakazojikita katika kulinda amani, kuheshimu utu, na kuepuka matusi au udhalilishaji dhidi ya washindani wao.
"Tutatumia hoja kunadi sera zetu. Ilani yetu imebeba majawabu kwa changamoto za nchi na matumaini kwa Watanzania wote. Tunavikaribisha hata vyama vingine vije kusikiliza," alisema Kihongosi. Aliongeza kuwa baada ya Dar es Salaam, msafara wa kampeni utaelekea mkoani Morogoro na kisha makao makuu ya nchi, Dodoma.
Wakati CCM ikijinadi kwa kampeni za amani, vyombo vya dola vimeonesha msimamo mkali kuhusu usalama katika kipindi chote cha uchaguzi. Jeshi la Polisi nchini, kupitia kwa msemaji wake Naibu Kamishna David Misime, limetoa onyo kali kwa wagombea na wafuasi wao, likitahadharisha kuwa halitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayekuwa chanzo cha vurugu au uvunjifu wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Msimamo huo umeungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ambaye amevihakikishia vyama vyote vya siasa ulinzi wa kutosha. Hata hivyo, alionya kuwa serikali haitavumilia mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga amani. "Yeyote atakayekuwa katikati ya kuharibu amani, wajibu wangu na wa vyombo vya dola ni kumdhibiti ili asikwamishe mchakato wa uchaguzi," alisisitiza Chalamila.
Mkuu huyo wa mkoa pia aliwataka wananchi kuwa makini na maneno ya wanasiasa katika kipindi hiki, akiwahimiza kuwapima wagombea kwa sera zao ili wafanye maamuzi sahihi siku ya kupiga kura.