Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kupokea wanachama wapya katika mkoa wa Lindi, hasa katika wilaya mbili, ambao wameripotiwa kutoka Chama cha Wananchi (CUF).
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, alipokuwa akizungumza na wananchi katika Wilaya ya Kilwa tarehe 10 Aprili na Liwale tarehe 11 Aprili 2025, aliwapokea wanachama hao wapya ambao walirejesha kadi zao za CUF na kujiunga na CCM.
Katika Wilaya ya Kilwa, zaidi ya wanachama wapya 70, wakiongozwa na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kupitia CUF, Bwana Vedasto Ngombale, walipokelewa rasmi. Walieleza kuwa sababu kubwa ya wao kuhamia CCM ni kuridhishwa na utekelezaji wa ilani ya chama hicho, pamoja na maendeleo makubwa na mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa na serikali ya CCM.
Bwana Makalla aliwapongeza wanachama hao wapya kwa uamuzi wao wa kurejesha kadi zao na kujiunga na CCM. Aliwataka viongozi wa CCM katika ngazi ya Wilaya na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kuhakikisha wanafuata taratibu za kuwapatia kadi wanachama hao ili kukamilisha usajili wao na kuwa wanachama kamili wa CCM.
"Tumewapokea hapa aliyekuwa Mbunge, ndugu yangu, amerudi CCM na wenzake. Hapa walitakiwa kuwa 70, lakini wameongezeka na kuwa zaidi ya 70. Ninawaelekeza katibu wa wilaya na mkuu wa wilaya tengenezeni utaratibu wa kuwapatia kadi hawa wanachama wapya," alisema Bwana Makalla.
Aliongeza: "Hili ni jeshi kubwa linalokuja kuongeza ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi. Wengine baada ya kunikabidhi kadi wamenipa na mihuri kabisa, maana yake wamefunga ofisi. Katibu, utaiangalia hii mihuri, tuweke kwenye kumbukumbu zetu."
Aliwataka viongozi wa CCM katika mkoa huo kuwatumia vizuri wanachama hao wapya katika wilaya zao, akisisitiza kuwa Bwana Ngombale na wenzake bado wana nguvu kama walivyoeleza. Hivyo, aliwashauri viongozi kuwatumia vizuri kwa manufaa ya chama.
Katika hatua nyingine, ndani ya Wilaya ya Liwale, wanachama wawili ambao waliwahi kugombea katika uchaguzi uliopita kupitia CUF, Bwana Hamis Kilaya na Bwana Shaban Kimbinga, nao walijiunga na CCM.