Morogoro Mpya: Matengo 'Atesa' kwa Kura za Kishindo, Thabit Apita Tundu la Sindano U-Naibu Meya

politics | Mon Dec 01 2025


Morogoro Mpya: Matengo 'Atesa' kwa Kura za Kishindo, Thabit Apita Tundu la Sindano U-Naibu Meya

Joto la kisiasa lililokuwa limetanda katika viunga vya Manispaa ya Morogoro, maarufu kama 'Mji Kasoro Bahari', hatimaye limetulia baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukamilisha mchakato wake wa demokrasia ya ndani na kuwapata manahodha wapya watakaoliongoza Baraza la Madiwani kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2025-2030).


Zoezi hilo la uchaguzi lililofanyika leo katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kata ya Kingo, limeshuhudia mchuano wa aina yake huku sura mpya zikiaminiwa kushika hatamu za kuiletea maendeleo manispaa hiyo kongwe nchini. Katika kinyang'anyiro cha Umeya, Diwani wa Kata ya Mji Mkuu, Bw. Khalid Mohamed Matengo, ameibuka kidedea kwa ushindi wa "Sunami" uliowaacha wapinzani wake wakishangaa.


Ushindi wa 'Kishindo' kwa Matengo Matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo yamebainisha kuwa Khalid Matengo amechaguliwa kuwa Mstahiki Meya mpya baada ya kuzoa kura 34 kati ya 39 zilizopigwa na wajumbe halali. Ushindi huu wa zaidi ya asilimia 85 unaashiria imani kubwa ambayo madiwani wa CCM wameweka kwake.


Wapinzani wake katika nafasi hiyo walipata wakati mgumu, ambapo Milikiel Michael Mansuet aliambulia kura 3 huku Richard Severine Mmanda akipata kura 2 pekee. Ushindi huu unamtviska Matengo jukumu zito la kuibadili Morogoro kuwa jiji la kibiashara na kitalii kama ilivyo azma ya serikali.


Naibu Meya Apita "Tundu la Sindano" Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kabisa katika nafasi ya Naibu Meya ambapo mchuano ulikuwa mkali na wa kukata na shoka. Diwani wa Kata ya Boma, Bw. Mohamed Thabit, alilazimika kusubiri hadi kura ya mwisho kuhesabiwa ili kutangazwa mshindi. Thabit amepata kura 20, akimshinda kwa kura moja pekee mpinzani wake wa karibu, Bi. Latifa Ganzel, aliyepata kura 19. Ushindi huu mwembamba unaashiria kuwa Naibu Meya huyo ana kazi kubwa ya kuunganisha madiwani ili wazungumze lugha moja ya maendeleo.


Ahadi za Viongozi Wapya Akizungumza kwa unyenyekevu mara baada ya kutangazwa mshindi, Meya Mteule Matengo amewashukuru wajumbe kwa kumpa ridhaa hiyo na kuahidi kuwa uongozi wake utajikita katika uwazi, ukweli, na ushirikiano.


"Ndugu zangu, kura hizi ni deni. Nimejipanga kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo. Kipaumbele changu ni kuboresha huduma za msingi zinazomgusa mwananchi wa kawaida, hasa maji safi na salama, huduma za afya, elimu bora, na ustawi wa jamii. Tutatatua changamoto za Manispaa yetu kwa kufuata miongozo ya chama na serikali," alisisitiza Matengo.


Kwa upande wake, Naibu Meya mpya, Mohamed Thabit, ameahidi kuwa kiungo imara (daraja) kati ya Baraza la Madiwani na watumishi wa Halmashauri ili kuhakikisha maagizo na mipango inatekelezwa kwa wakati.


Rai ya Madiwani kwa Uongozi Mpya Wakitoa maoni yao baada ya uchaguzi huo, baadhi ya madiwani wamewataka viongozi hao kutobweteka. Diwani wa Viti Maalum, Bi. Batuli Kifea, ambaye ni sura mpya katika baraza hilo la 2025–2030, amewapa "nondo" viongozi hao.


"Tunataka kuona Morogoro mpya. Viongozi hawa wahakikishe wanaimarisha miundombinu ya barabara za mitaani, wanaboresha hospitali zetu na kuifanya Manispaa hii kuwa ya kisasa inayovutia uwekezaji. Sisi tupo tayari kushirikiana nao bega kwa bega," alisema Kifea.


Uchaguzi huu unahitimisha safu ya uongozi wa juu wa Halmashauri hiyo, huku wananchi wa Morogoro wakisubiri kwa hamu kuona utekelezaji wa ahadi hizo katika kuboresha maisha yao ya kila siku.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.