Mkakati wa Nishati Safi kwa Vitendo: Maafisa Magereza Iringa Sasa Kula kwa Gesi Baada ya Taasisi Yao Kuaga Kuni

politics | Thu Jul 10 2025


Mkakati wa Nishati Safi kwa Vitendo: Maafisa Magereza Iringa Sasa Kula kwa Gesi Baada ya Taasisi Yao Kuaga Kuni

Katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendeleza wimbi la mapinduzi ya nishati kwa kuwakabidhi mitungi 366 ya gesi ya kupikia na majiko yake kwa watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Iringa.


Hatua hii ni mwendelezo wa mradi mkubwa ambao awali uliwezesha magereza yote nchini kuachana na matumizi ya kuni na kuanza kutumia nishati safi, ikiwa ni sehemu ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa nchi inayotumia nishati rafiki kwa mazingira na afya.


Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Florian Haule, alisema kitendo cha kuwapa nishati safi watumishi hawa ni hatua ya pili baada ya kufanikiwa kuwapatia nishati hiyo kwenye maeneo yao ya kazi.


"Tunawapongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuibeba ajenda hii kwa uzito mkubwa. Alitoa fedha zilizowezesha magereza kama taasisi kuondokana na kuni. Leo, tunawaletea nishati hii majumbani kwenu watumishi. Hii inadhihirisha dhamira ya serikali ya kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034," alisema Haule.


Mradi huu mpana kati ya REA na Jeshi la Magereza, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 35.23, unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya nishati safi katika magereza zote nchini.


Kaimu Meneja wa REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya, aliwataka watumishi hao wa magereza kuwa mabalozi wazuri wa matumizi ya nishati safi katika jamii zao. "Ninyi sasa ni mfano wa kuigwa. Tunawaomba mtunze vifaa hivi na muwe mabalozi wa kuhamasisha wengine kuachana na mkaa na kuni," alisema Mhandisi Yesaya.


Akipokea msaada huo, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ackles Haule, aliishukuru serikali na REA, akiahidi kuwa watumishi wake watakuwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira na kuunga mkono ajenda hii ya kitaifa kwa vitendo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.