Furaha na faraja vimetawala miongoni mwa watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoani Geita baada ya kupokea msaada wa majiko na mitungi ya gesi ya kupikia kutoka serikalini, hatua waliyoielezea kama ukombozi kutoka kwa adha ya nishati ya mkaa na kuni. Jumla ya watumishi 310 wamepatiwa bure seti kamili ya mtungi wa gesi wa Kilogramu 15 na jiko la sahani mbili kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
"Mimi kama mama na mtumishi, kuna muda nachelewa kurudi kazini. Sasa hata nikichelewa, naweza kuandaa chakula kwa familia yangu kwa haraka zaidi. Nina furaha sana," alisema Koplo Leonida, akielezea faida za haraka za nishati hiyo safi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Geita, ACP Jonam Mwakasagule, alisema hii ni baraka ya pili kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alieleza kuwa serikali ilishafanikiwa kuondoa matumizi ya kuni ndani ya magereza yote nchini, na sasa imewakumbuka watumishi majumbani mwao.
"Kwanza, matumizi ya kuni magerezani yamekuwa historia. Sasa Mheshimiwa Rais ametukumbuka na sisi watumishi wake binafsi. Haya ni mapenzi ya kipekee, tunamshukuru sana," alisema ACP Mwakasagule.
Ugawaji huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde, alisema REA inaendelea na jukumu la kuhamasisha na kuwezesha wananchi kuachana na nishati zinazoharibu mazingira na afya.
Watumishi waliopokea msaada huo wameahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha jamii inayowazunguka kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi. Wamesema mbali na kuokoa muda, nishati ya gesi itawalinda na magonjwa yatokanayo na moshi wa kuni na mkaa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Emmanuel Yesaya kutoka REA, watumishi wote 310 wa Magereza mkoani Geita watanufaika na mpango huu, ambao ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha maisha ya watumishi wa umma na kulinda mazingira kwa vitendo.