Kifo cha kutisha kimemkumba mfanyabiashara mashuhuri wa nyama katika soko la Mawenzi, mjini Morogoro, Bw. Masaka, mkazi wa Mkundi, ambaye mwili wake umepatikana ukiwa umetupwa kikatili katika Kijiji cha Manga, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga. Tukio hili la kusikitisha limetokea baada ya Bw. Masaka kutoweka tangu Juni Mosi, 2025, na kusababisha hofu na simanzi kubwa mkoani Morogoro na maeneo jirani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amethibitisha kutokea kwa mauaji haya ya kutisha na kueleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea. Tayari watu saba wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo, wakiwemo wafanyabiashara wenzake wa marehemu. Chanzo cha mauaji haya kinadaiwa kuwa ni wivu wa kibiashara, hasa kutokana na usimamizi mkali wa marehemu katika kudhibiti uingiaji wa nyama isiyo rasmi sokoni.
Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limefanya kazi kwa weledi mkubwa kufichua ukweli wa tukio hili. Uchunguzi wao umefanikiwa kubaini kuwa Bw. Masaka alitekwa nyara na kuuawa kikatili kabla ya mwili wake kutelekezwa mkoani Tanga, juhudi zilizolenga kuficha uhalifu huo. Miongoni mwa wanaoshikiliwa na polisi ni Stanley Ng’ambi maarufu Jaha (31), Japhet Michael (29), Robson Rite (47) na Ernest Charles maarufu Chief (37), wote wafanyabiashara wakazi wa Mkundi na Sabasaba Morogoro. Wengine ni Yusuph Mkamba (27) dereva bodaboda mkazi wa Msamvu, na Nickson Ibrahim (43) fundi ushoni mkazi wa Kibamba, Dar es Salaam, akionyesha jinsi mtandao huu wa uhalifu ulivyokuwa mpana.
Uchunguzi wa awali umefichua kuwa Juni Mosi, 2025, Bw. Masaka alitekwa nyara na mtuhumiwa Stanley Ng’ambi na wenzake, kwa kumlaga kuwa wanakwenda eneo la Makunganya kununua ng'ombe wa biashara. Mara tu alipoingia ndani ya gari, aliuawa kikatili kwa kutumia vitu vyenye ncha kali, na baadaye mwili wake ukatupwa Handeni, Tanga. Kitendo hiki kinaashiria mpango mkakati wa kumuondoa Masaka, ambaye alionekana kama kikwazo kwa biashara haramu ya nyama.
Waandishi wa habari walipofika nyumbani kwa marehemu eneo la Mkundi, walikuta mwili ukiwa umewekwa kwenye basi dogo aina ya Costa, huku waombolezaji wakigoma kuzungumza na vyombo vya habari kutokana na simanzi kubwa. Hata hivyo, mwili uliondolewa majira ya saa tisa usiku kuelekea Matumbulu, mkoani Dodoma, kwa ajili ya taratibu za mazishi. Awali, mwili huo ulikuwa umezikwa Tanga baada ya kuokotwa na kukosa ndugu, lakini ulifukuliwa baada ya watuhumiwa kuonesha mahali walipoutupa.
Baadhi ya wafanyabiashara wenzake wa marehemu, waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao, walieleza kuwa Bw. Masaka alikuwa mtu mwema, mtaalamu wa biashara na kiongozi mahiri. Walidai alikuwa akidhibiti vikali uingiaji holela wa nyama isiyo rasmi sokoni, akichukua jukumu ambalo hata askari polisi walimtegemea. "Alikuwa zaidi ya Polisi, hata polisi wenyewe walimtegemea kwa mengi, aliwadhibiti vikali wafanyabiashara hawa wengine waliokuwa wanaingiza nyama za magendo sokoni na alifanikiwa, mji ulitulia," alisema mmoja wa wafanyabiashara.
Waliongeza kuwa Bw. Masaka alipotea tangu Juni Mosi, na uchunguzi wa awali wa polisi ulibaini mawasiliano yake ya mwisho yalifanyika na dereva wa mmoja wa wafanyabiashara wenzake. Dereva huyo, ambaye anadaiwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa, alipobanwa alikiri kuuawa kwa mfanyabiashara huyo na bosi wake, ingawa alikataa kuwaonesha polisi mahali mwili ulipokuwa na kutelekeza gari kwa bosi wake.
"Hawa waliohusika sio wafanyabiashara wepesi, wako vizuri kifedha na tunaamini kumuua Ben (Bernad) ilikuwa ni kumziba mdomo, manake wote walimuogopa kwa usimamizi wake makini kuthibitisha nyama ya magendo kuingia sokoni," alisema mfanyabiashara mwingine. Kifo chake kimeacha simanzi kubwa kwa wafanyabiashara wote wanaofuga na kuuza nyama kihalali, kwani alikuwa tegemeo na aliyekuwa anawafahamu wezi wote wa ng'ombe.
Wananchi mbalimbali wameeleza kusikitishwa na vitendo vya ukatili vilivyoshika kasi na kuitaka serikali kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na mauaji hayo, wakisisitiza umuhimu wa kurejesha hofu ya Mungu na utawala wa sheria. Tukio hili linapaswa kuwa funzo kwa jamii nzima kuhusu hatari za wivu wa kibiashara na umuhimu wa kuheshimu sheria.