Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, ametoa agizo kali akisema hataki kusikia tena malalamiko kuhusu ukosefu wa dawa katika Hospitali ya Utete. Alimtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Hamis Abdallah, kuhakikisha anashughulikia tatizo hilo kwa haraka ili wananchi waendelee kupata huduma bora za afya.
Mchengerwa alitoa maelekezo hayo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya wakati wa ziara yake ya kikazi katika Hospitali ya Wilaya ya Rufiji, iliyopo Utete, ambapo alisisitiza uwajibikaji.
"Mganga Mkuu, umepewa nafasi ya kufanya kazi Rufiji, kwa hiyo unapaswa kushirikiana na wasaidizi wako ili kumaliza tatizo la ukosefu wa dawa katika eneo hili, ambalo mimi kama Waziri wa TAMISEMI ninalisimamia," alisisitiza Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa alieleza kuwa Rufiji haijawahi kukumbana na changamoto kama hiyo ya kukosa dawa hapo awali, akitoa mfano wa kipindi ambacho Dk. Makenge alikuwa Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo.
"Mganga Mkuu, jambo hili halipendezi. Sitaki kusikia wananchi wakilalamika tena kuhusu kukosa dawa. Panga mikakati kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana kila wakati, na nitaanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha tatizo, kwani Serikali haina shida ya fedha kwa ajili ya dawa," aliongeza Mchengerwa.
Pamoja na hayo, Mchengerwa aliwapongeza Waganga Wakuu na watumishi wote wa sekta ya afya kwa kazi nzuri wanayofanya katika kupunguza vifo vya mama na mtoto na kudhibiti vitendo vya rushwa, hasa dhidi ya wanawake wanaokwenda kupata huduma za afya ya uzazi katika hospitali na vituo vya afya nchini.
Kwa upande wake, Mwema Said, mmoja wa wananchi wa Wilaya ya Rufiji, alimshukuru Waziri Mchengerwa kwa kuboresha miundombinu katika hospitali hiyo. Alisema kuwa kwa sasa wananchi wanafurahia wodi mpya, vifaa tiba vilivyonunuliwa, pamoja na huduma bora zinazotolewa.