Kasi ya ukuaji wa mji wa Kibaha, ambao ndio lango kuu la kuingia jijini Dar es Salaam na kitovu cha viwanda mkoani Pwani, imekuja na changamoto zake, kubwa ikiwa ni migogoro ya ardhi na upangaji wa miji. Ili kukabiliana na 'jipu' hili linalowakosesha usingizi wananchi na wawekezaji, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, ameamua kuongeza nguvu ya 'mapambano' kwa kukabidhi vitendea kazi vya kisasa.
Katika hafla fupi lakini yenye uzito iliyofanyika Desemba Mosi katika viunga vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, DC Simon amekabidhi gari jipya (brand new) kwa Kitengo cha Ardhi na Mipango Miji. Gari hilo, ambalo ni la kisasa na linaloendana na mazingira ya kazi za 'field', limetajwa kuwa na thamani ya Shilingi Milioni 170.
"Gari Hili Siyo la Harusi, ni la Shamba" Akizungumza kwa msisitizo wakati wa makabidhiano hayo, DC Simon ameweka wazi kuwa serikali haijanunua gari hilo kwa ajili ya anasa za watumishi, bali kama "silaha" ya kuwafikia wananchi huko waliko—kwenye mashamba, viwanja na mipaka yenye utata.
"Hili gari limeletwa kwa kazi maalum; kuwafikia wananchi kwa haraka na kumaliza kero zao. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan hataki kusikia mwananchi anazungushwa ofisini eti kisa hakuna usafiri wa kwenda site kupima. Itunzeni na mlitumie kuhakikisha vikwazo vya ardhi vinatatuliwa kwa wakati ili wawekezaji wapate maeneo ya viwanda bila bughudha," alisisitiza DC Simon.
Kiongozi huyo alimwaga sifa kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Dk. Rogers Shemwelekwa, kwa ubunifu na utekelezaji wa maagizo ya Rais kwa vitendo, akisema kuwa uwekezaji huo utalipa kwa kuongeza mapato ya halmashauri kupitia kodi za ardhi zilizokuwa zinapotea.
Kibaha Kama Kitovu cha Uwekezaji Mkurugenzi Dk. Shemwelekwa alifafanua kuwa ununuzi wa gari hilo la milioni 170 ni mkakati wa kimakusudi wa kuendana na kasi ya ukuaji wa mji huo. Kibaha sasa inavutia wawekezaji wengi wa viwanda na makazi, hivyo Idara ya Ardhi ndiyo moyo wa mipango hiyo. "Hii ni nyenzo muhimu sana. Kasi ya utoaji huduma sasa inaenda kuongezeka maradufu," alieleza Dk. Shemwelekwa.
Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani, Bw. Rugambwa Banyikila, alieleza kuwa hatua hiyo imekuja wakati muafaka. Alitoa rai kwa watumishi wa ardhi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake watumie usafiri huo kumaliza viporo vya migogoro ambayo imekuwa ikichafua taswira ya mkoa huo.
"Hakuna Kisingizio Tena" Kwa upande wa watendaji, Mkuu wa Kitengo cha Ardhi, Bw. Denis Kahumba, amepokea "chuma" hicho kwa mikono miwili, akikiri kuwa changamoto ya usafiri ilikuwa kikwazo kikubwa katika utendaji wao wa kila siku.
"Tunamshukuru Mkurugenzi na DC kwa kutujali. Ahadi yangu ni moja tu; tutatoa huduma bora zaidi. Hapa sasa hakuna kisingizio, morali ya watumishi imepanda na tutahakikisha kila mwananchi anapata haki yake ya ardhi kwa wakati," aliahidi Kahumba.
Upatikanaji wa gari hili unatazamwa kama hatua muhimu ya kuimarisha utawala bora na kuboresha mazingira ya biashara (Doing Business Environment) katika Manispaa ya Kibaha, eneo ambalo linaendelea kuwa kimbilio la wakazi wa Dar es Salaam na wawekezaji wa kimataifa.