Katika kuhakikisha fedha za walipa kodi haziliwi na mchwa wala kupotea kwenye miradi hewa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, ameamua kuvaa gwanda na ‘kushuka site’ kukagua miradi, huku akitoa onyo kali kwa watendaji wenye tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
Hatua hiyo imekuja wakati ambapo Manispaa hiyo, ambayo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani, inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mji huo ambao ni lango kuu la kuingia jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika ziara hiyo iliyolenga "kufukua" changamoto na kupima kasi ya utekelezaji, Dk. Shemwelekwa amesisitiza kuwa zama za miradi kukwama au kujengwa chini ya kiwango zimepita. Aliwataka watendaji wa Halmashauri hiyo 'kujiongeza' na kusimamia miradi hiyo kwa jicho la tai ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha (Value for Money).
"Tunataka miradi hii iwe mkombozi kwa wananchi wetu, siyo kero. Kila shilingi iliyotolewa na Serikali lazima ionekane. Sitavumilia kuona miradi inasuasua wakati fedha zipo," alisisitiza Dk. Shemwelekwa kwa ukali.
Akiwa katika Kata ya Kongowe, eneo ambalo linakua kwa kasi kibiashara na makazi, Mkurugenzi huyo alitembelea Shule ya Msingi Mwambisi. Shule hii, ambayo ni ya mchepuo wa Kiingereza (English Medium), imetajwa na Dk. Shemwelekwa kama "Lulu" na kielelezo cha ufanisi ndani ya Manispaa hiyo.
Akishuhudia mandhari safi, nidhamu ya hali ya juu, na usimamizi madhubuti wa taaluma katika shule hiyo, Dk. Shemwelekwa amezitaka shule nyingine zote za serikali ndani ya Kibaha kuacha "kupiga mark-time" na badala yake ziende kujifunza siri ya mafanikio kutoka Mwambisi.
"Shule zinazosuasua kitaluma hazina budi kujitathmini. Kwanini Mwambisi wanaweza? Lazima mbadilishane uzoefu. Hatutaki kusikia visingizio wakati wenzenu wanafanya maajabu kwenye mazingira hayahaya," alieleza.
Aidha, ziara hiyo iliigusa pia Shule ya Msingi Kongowe Bamba, ambapo Dk. Shemwelekwa alimwaga sifa kwa walimu wa shule hiyo kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo. Hatua hii inaakisi jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imekuwa ikimwaga fedha nyingi kuboresha miundombinu ya elimu ili kuondoa msongamano madarasani.
Kibaha, ikifahamika kihistoria kama kitovu cha elimu nchini (ikikumbukwa kwa Shule ya Sekondari Kibaha na Kituo cha Elimu Kibaha - KEC), ina jukumu kubwa la kulinda hadhi hiyo. Hivyo, msukumo wa Dk. Shemwelekwa unalenga kurudisha heshima ya elimu katika mkoa wa Pwani.
Katika ziara hiyo iliyoshirikisha wakuu wa idara na vitengo mbalimbali, timu hiyo ilipita pia kwenye vituo vya afya na miradi mingine ya miundombinu inayotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani ya Halmashauri, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha Kibaha inakuwa Manispaa ya mfano nchini.