Katika jitihada za kulinda heshima na uadilifu wa taaluma ya sheria nchini, Kamati ya Mapambano dhidi ya Vishoka, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Wakili Sweetbrt Nkuba, imewataka wananchi kuwa makini na kutumia huduma za mawakili waliothibitishwa pekee. Wito huu unakuja kufuatia ongezeko la watu wanaojitambulisha kama watoa huduma za kisheria kwa bei nafuu, huku wakiwa hawana sifa wala leseni halali. Aidha, amesisitiza umuhimu wa mashirika ya umma na binafsi kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika kuwakagua kwa umakini wanaojihusisha na kazi za kisheria, ili kutokomeza kabisa tabia za utapeli zinazodhoofisha taaluma.
Wakili Nkuba aliyasema hayo leo Juni 17, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni kabambe ya kutokomeza vishoka wa uwakili nchini, na pia kujadili masuala ya malipo ya mawakili. Alieleza kuwa changamoto ya vishoka imekuwa kubwa na inaathiri wananchi wengi. "Kwa masikitiko makubwa, tumeshuhudia ongezeko la watu wanaojihusisha na utoaji wa huduma za kisheria bila kuwa mawakili. Hawa huitwa vishoka na matendo yao ni kinyume cha sheria," alisisitiza Wakili Nkuba.
Vishoka ni Akina Nani na Wanaathirije Jamii?
Wakili Nkuba alifafanua aina mbalimbali za vishoka, akianza na wale waliowahi kuwa mawakili lakini hawajahuhisha leseni zao kwa mwaka husika (Non-Practicing Members), au wale waliofungiwa kutoa huduma lakini wanaendelea kujihusisha na uwakili. Alisema kuwa kujihusisha kwao na huduma za uwakili bila uhalali ni kinyume cha sheria, na mbaya zaidi, baadhi yao wanatumia mihuri bandia au kughushi mihuri ya mawakili halali ili kuwadanganya wananchi.
"Kitendo hiki ni kosa la jinai linaloathiri uaminifu wa nyaraka za kisheria. Kumekuwa na wimbi la mawakili wasio waaminifu wanaoruhusu watu wasio mawakili kutumia mihuri yao kuthibitishia nyaraka au kutoa viapo," alisema Nkuba, akifafanua jinsi tabia hizi zinavyochangia kuzorota kwa mfumo wa haki. Aliongeza kuwa suala hili limesababisha kuwepo na wimbi la wahalifu kuchonga mihuri na kuitumia kama mawakili, jambo linaloshuhudiwa katika maeneo mbalimbali yanayohitaji huduma ya mawakili kama vile Uhamiaji, NIDA, na ofisi zingine za serikali.
Umuhimu wa Kuwatumia Mawakili Halali
Wakili Nkuba aliwakumbusha wananchi kuwa nyaraka yoyote iliyowekwa muhuri wa wakili na mtu asiye wakili ni ya kughushi na ni batili, iwe ni kiapo au mkataba. Alihimiza wananchi kwenda kwa mawakili halali ili kuepuka matatizo ya kisheria yanayoweza kujitokeza kutokana na nyaraka bandia. Alishangazwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuwa tayari kumlipa dalali hadi asilimia 10 ya bei ya manunuzi ya nyumba au kiwanja, lakini wanaona kutoa asilimia tatu au sita kwa wakili kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa kama sio stahili. Alisisitiza kuwa wakili ndiye anayehakikisha uhalali wa makubaliano husika, jambo linaloleta usalama wa kisheria.
Aidha, Wakili Nkuba aliziomba mamlaka za usalama kuongeza juhudi katika kuwakamata na kuwafungulia mashtaka vishoka. Pia, alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaotoa huduma za kisheria bila usajili au kwa kutumia nyaraka bandia. Alihitimisha kwa kusema kuwa tabia hizi potofu zinaathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya taaluma ya sheria na taifa kwa ujumla, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika ili kuzitokomeza. Kampeni hii ni muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa mfumo wa haki na kuhakikisha huduma za kisheria zinatolewa kwa uaminifu na weledi.