Mgombea urais kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Bw. Doyo Hassan Doyo, amewaahidi wakazi wa Jiji la Tanga kwamba, endapo atachaguliwa, jambo la kwanza atakalofanya ni kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria viongozi wote wa Serikali waliohusika na ubadhirifu wa fedha za ujenzi na ukarabati wa masoko makuu ya jiji hilo.
Akizungumza kwa hisia kali leo, Oktoba 26, na wafanyabiashara na wakazi wa Jiji la Tanga, Doyo alitaja masoko yanayohitaji kipaumbele kuwa ni Mgandini, Makorola na Mlango wa Chuma. Alieleza kusikitishwa kwake kwa jinsi masoko hayo yalivyotengewa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati siku za nyuma, lakini fedha hizo zote "hazijulikani zilikokwenda," huku masoko hayo yakibaki katika hali ya uchakavu isiyofaa kuitwa masoko ya Jiji la kisasa.
“Haya masoko matatu yalishatengewa fedha, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Masoko ni machakavu, hayafai.
Nikiingia madarakani, nitakwenda kuwashughulikia wote waliozitafuna hizi hela maana ni mabilioni ya pesa,” alisisitiza Doyo, akiahidi uwajibikaji mkubwa katika serikali yake.
Doyo ameahidi kwamba Serikali yake itahakikisha masoko yote matatu yanajengwa upya, na yatajengwa kwa ghorofa tatu ili kulipa jiji la Tanga hadhi ya kuwa la kisasa. Lengo ni kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanga kufanya biashara zao katika mazingira ya hadhi na yaliyo huru kutokana na changamoto za sasa, huku wakitumia msemo usemao, "Mpiga ngoma kwa nguvu zake, ngoma inalia kwa sauti yake."
Akifafanua muundo wa masoko hayo mapya, Doyo alisema ghorofa ya chini itatengwa kwa ajili ya wauzaji wa mbogamboga, ghorofa ya katikati itakuwa kwa ajili ya wafanyabiashara wa mchele na nafaka, huku ghorofa ya juu ikiwapokea wafanyabiashara wa nyanya na bidhaa zingine. Muundo huu utamwezesha mnunuzi yeyote kufika sokoni na kumaliza shughuli zake zote za manunuzi katika eneo moja.
“Sokoni si sehemu ya kuuza tu mbogamboga na nyanya, bali ni kituo cha biashara zote. Mkinichagua kuwa Rais, tutakwenda kujenga soko la biashara lenye hadhi na meza za kisasa na ninyi muwe watu wenye heshima katika biashara zenu,” alihitimisha Doyo.