Kampeni za Uchaguzi Mkuu zikielekea ukingoni, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amewateka Watanzania wa Kanda ya Ziwa kwa hoja ya utendaji badala ya maneno. Ziara yake katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga, na Simiyu imeonyesha mafanikio makubwa yaliyofanyika, na wengi wa wananchi wamempa sifa ya kuwa ‘Kiongozi Mwenye Dira na Uhalisia’.
Katika mikutano yake mikubwa, Dk. Samia ametoa na kutekeleza zaidi ya ahadi 50 ambazo zimegusa sekta muhimu za uchumi na kijamii. Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, Katibu Mkuu wa CCM, alimtambulisha Dk. Samia kama kiongozi wa matendo, akisisitiza kuwa ahadi zake zinapimika na kazi zake zinaonekana.
Maboresho Makubwa Kwenye Sekta za Jamii
Katika sekta ya afya, mgombea huyo wa CCM ameeleza mafanikio ya Hospitali ya Rufani ya Kagera, ambapo huduma za kibingwa zimeimarishwa, na hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kusafiri kwenda Bugando au Muhimbili. Takwimu zinaonyesha ongezeko la wagonjwa waliopata tiba hapo, kutoka 128,305 mwaka 2021 hadi 478,002 mwaka 2025 – ongezeko la zaidi ya watu 349,000. Ahadi kubwa zaidi iliyopokewa kwa vigelegele ni uzinduzi wa bima ya afya kwa wote ndani ya siku 100 za kuchaguliwa tena, ili kuondoa vikwazo vya kiuchumi katika matibabu.
Kwa upande wa elimu, serikali ya Samia imeendelea kujenga shule mpya, mabweni, na vyuo vya ufundi (VETA). Kagera pekee ina shule tatu za amali, shule ya sayansi ya wasichana, na vyuo vitano vya VETA vilivyojengwa katika miaka mitano iliyopita. Aidha, Mfuko wa Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) umeendelea kutunishwa ili kutoa fursa kwa vijana wengi wa kitanzania kujiendeleza, kwa lengo la kufanya elimu iwe nguzo ya ajira na ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Kuimarisha Biashara na Uwezeshaji Kiuchumi
Akiwa Bukoba, Dk. Samia alitangaza ujenzi wa soko la kisasa la machinga complex lenye thamani ya Sh. bilioni 10, lengo likiwa ni kuimarisha mazingira ya biashara, kuongeza ajira, na kukuza mapato ya halmashauri. Vilevile, aliweka msisitizo kwenye mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu, na akasisitiza ahadi yake ya Sh. bilioni 200 kwa ajili ya mikopo mikubwa zaidi ya wajasiriamali, huku akisisitiza matumizi mazuri ya mikopo hiyo kwa miradi yenye tija.
Miundombinu na Nishati
Katika sekta ya nishati, ahadi kuu ni kuhakikisha kitongoji chochote ambacho bado hakijapata umeme kinapata huduma hiyo ndani ya miaka miwili ijayo. Kagera inajivunia miradi minne mikubwa ya kuzalisha umeme wa maji yenye jumla ya Megawati 221.8, ikiwemo Rusumo na Ngara. Pia, juhudi za kusambaza nishati safi ya kupikia zinaendelea kwa kasi ili kulinda mazingira na afya za wananchi.
Mageuzi ya Kilimo na Usafirishaji
Dk. Samia amesema Serikali imejipanga kuibadili sekta ya kilimo kutoka kilimo cha mazoea na kuwa kilimo biashara kupitia mpango wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT). Mpango huu unalenga kuwapa vijana, wavuvi, na wafugaji mitaji na vifaa vya kisasa. Viwanda vya kuongeza thamani ya mazao kama kahawa na samaki vitaendelea kujengwa Kanda ya Ziwa, huku bandari za uvuvi, vituo vya kuhifadhia samaki, na machinjio vikiboreshwa kufikia viwango vya kimataifa ili kuongeza mauzo nje.
Uboreshaji wa Bandari ya Kemondo na ya Bukoba na kuongezeka kwa usalama wa mizigo na abiria ni sehemu ya mikakati ya kukuza biashara na nchi jirani za Uganda na Rwanda. Kilele cha mafanikio ni kukamilika kwa meli ya kisasa ya MV Mwanza, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400, ambayo itakuwa chachu ya biashara na utalii katika Ziwa Victoria.
Siasa na Umoja
Kampeni za Dk. Samia zimeambatana na matukio ya kihistoria, ikiwemo kurejea kwa viongozi wa upinzani ndani ya CCM. Ezekia Wenje, Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA Kanda ya Victoria, alirudi CCM akisema, “mbele kuna mwanga,” akisisitiza kwamba “Mheshimiwa Samia ametenda” na miradi ya mabilioni inaonekana kila kona. Kauli hii inashadidiwa na wananchi kama Neema Byabato, mkazi wa Bukoba, ambaye anasema: “Tunaona matokeo, si propaganda. Hii ni serikali inayotenda, si ya maneno.” Dk. Samia anahitimisha kwa kusisitiza umoja na amani kama msingi wa maendeleo yote.