Katika hatua ya kihistoria kwa mustakabali wa maendeleo ya Tanzania, Serikali imetangaza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 sasa imepata nguvu ya kisheria baada ya kupitishwa na Bunge, hatua inayoizuia kubadilishwa na rais yeyote bila idhini ya Bunge. Hii inamaanisha dira hiyo imewekewa "ngao ya kisheria" kuhakikisha utekelezaji wake hauathiriwi na mabadiliko ya kisiasa.
Akitangaza kukamilika kwa dira hiyo jana, Julai 8, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, alisema hatua hii, iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inatofautisha Dira 2050 na ile ya 2025 ambayo iliishia kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri pekee.
"Tumeiwekea ulinzi mkubwa kupitia Bunge. Hii ni sheria sasa. Rais yeyote akitaka kubadilisha lazima arudi bungeni. Yeyote aliyepo madarakani hawezi kuamua kuiacha," alisisitiza Prof. Mkumbo, akiongeza kuwa dira hiyo imeandaliwa kutekelezwa na Marais watatu tofauti.
Prof. Mkumbo alieleza kuwa Dira hiyo, itakayojulikana kama "Dira 2050: Tanzania Tuitakayo," ni matokeo ya mchakato mrefu na shirikishi wa hatua 13. Mchakato huo ulijumuisha tathmini ya kina ya Dira 2025, ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wananchi, na mashauriano na makundi mbalimbali yakiwemo vyama vya siasa na vyombo vya habari ili kujenga maridhiano ya kitaifa.
"Tulikubaliana na vyama vya siasa tusibishane juu ya tunakokwenda, bali ilani zetu ziakisi mwelekeo huu mmoja wa kitaifa," alisema. Aliongeza kuwa Tanzania imejifunza kutoka nchi zilizopiga hatua kubwa za maendeleo barani Afrika kama Botswana na Mauritius, na Asia kama Korea Kusini, China na Singapore.
Waziri huyo alivipongeza vyombo vya habari, akisema serikali inatambua kuwa uwajibikaji hauwezi kupatikana bila vyombo vya habari vilivyo imara. "Katika jamii iliyostaarabika, maana unaipata kutoka kwa walimu na waandishi wa habari. Anayedharau vyombo vya habari anakosea sana," alisema Prof. Mkumbo.
Dira ya Taifa 2050 itazinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Julai 17, 2025, na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza rasmi Julai 1, 2026.