Ikiwa ni wiki moja tu tangu Rais Samia Suluhu Hassan azindue rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sasa macho na masikio ya wadau wa maendeleo nchini yanaelekezwa jijini Mwanza, ambapo kongamano maalum la kitaaluma litafanyika kesho, Julai 26, 2025, kuweka ramani ya utekelezaji wa dira hiyo. Mada kuu mezani ni jinsi ya kutumia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kama injini kuu ya kufanikisha maono hayo.
Kongamano hili, linaloandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia Mpango wake wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP Centre), linatajwa kuwa hatua ya kwanza na muhimu zaidi ya kugeuza Dira ya 2050 kutoka kwenye makaratasi na kuipeleka kwenye utekelezaji.
Akizungumza kuhusu kongamano hilo, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa UDSM, Dk. Lupa Ramadhani, alisema uzinduzi wa Dira 2050 ulisisitiza wazi kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu, na kongamano hili linalenga kuchambua kwa kina jinsi ushiriki huo utakavyofanyika.
"Lengo ni kujenga uelewa wa pamoja na wa kimkakati kuhusu thamani ya PPP katika kufanikisha Dira ya Taifa. Tutachambua changamoto na fursa zilizopo, na kujenga mwafaka wa kitaifa wa jinsi ya kuoanisha miradi ya PPP na vipaumbele vya Dira 2050," alisema Dk. Lupa.
Alifafanua kuwa mjadala utajikita katika maeneo makuu matatu: nafasi ya PPP katika kukuza uwekezaji na ufanisi katika serikali za mitaa; dhana ya PPP katika muktadha mpana wa Dira 2050; na nafasi ya mitaji ya kimataifa na sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha PPP, Chelu Matuzya, alisema kongamano hilo la Mwanza litakuwa la uwazi na litatoa mwelekeo wa jinsi miradi yote ya kimkakati itakavyotekelezwa kwa ufanisi wa asilimia 100, likihusisha zaidi ya washiriki 300 kutoka serikalini, sekta binafsi, asasi za kiraia, na taasisi za elimu ya juu.