CHAUMMA: Tutafuta Bunge la 'Ndiyo Mzee', Wabunge Watakuwa Sauti ya Wananchi

politics | Tue Oct 14 2025


CHAUMMA: Tutafuta Bunge la 'Ndiyo Mzee', Wabunge Watakuwa Sauti ya Wananchi

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimeahidi kuleta mageuzi makubwa katika Mhimili wa Bunge endapo kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kikisema kitahakikisha bunge linarejesha heshima yake kama chombo huru na chenye mamlaka ya kuisimamia serikali kikamilifu. Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, John Mrema, wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea urais wao, Salum Mwalimu.


Akizungumza kwa lugha kali na ya moja kwa moja, Mrema alitamka wazi kuwa zama za kuwa na bunge ambalo ni dhaifu, lisilo na meno ("kibogoyo"), na ambalo kazi yake kubwa ni kupiga makofi kwa kila kitu kinacholetwa na serikali, zitafikia kikomo chini ya utawala wao. Alisema CHAUMMA haitaki bunge "kigoigoi" linaloshindwa kutetea maslahi ya umma, bali bunge lenye wabunge jasiri wanaopaza sauti za wananchi bila woga.


"Kwa mujibu wa ilani yetu ya uchaguzi, ukurasa wa 10, tunatambua bunge kama mhimili mkuu wa kuiwajibisha serikali. Hivyo, serikali ya CHAUMMA itawapa wabunge wake uhuru kamili wa kuhoji, kukosoa, na kuibua hoja za msingi kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania wanaowawakilisha," alifafanua Mrema.


Alisisitiza kuwa mbunge chini ya serikali yao atakuwa na jukumu la msingi la kushauriana na wapiga kura wake kabla ya kuhudhuria vikao vya bunge. "Tunataka mbunge, kabla ya kuja Dodoma, afanye kwanza mikutano jimboni kwake, akusanye kero na maoni ya wananchi. Sauti itakayosikika bungeni iwe ni sauti halisi ya mwananchi wa kawaida, na si vinginevyo," aliongeza.


Mrema alihitimisha kwa kusema kuwa lengo lao kuu ni kurejesha mamlaka ya kikatiba ya bunge, ili liweze kuwa chombo kinachojitegemea na chenye nguvu ya kuhakikisha serikali inatekeleza majukumu yake kwa uwazi na kwa maslahi ya taifa zima.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.