bunge Asema Rais Samia Ni Dira ya Afrika, Ataka Bara Liwe Taifa Moja

politics | Fri Feb 14 2025


bunge Asema Rais Samia Ni Dira ya Afrika, Ataka Bara Liwe Taifa Moja

Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga, amemiminia sifa kedekede Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake zisizochoka katika kuleta maendeleo makubwa nchini. Akiwa bungeni jijini Dodoma, Hasunga alitoa wazo la kimapinduzi: kuunganisha Afrika kuwa taifa moja ili kuimarisha uchumi na kupunguza umasikini unaolikabili bara hili.


Akichangia hoja bungeni, Hasunga alisema kuwa umoja wa Afrika unaweza kuwa ufunguo wa bara hili kujitegemea kiuchumi, na kuachana na utegemezi wa misaada kutoka nje. "Afrika ina utajiri mkubwa wa rasilimali, lakini bado tunapambana na umasikini. Kama bara hili lingeungana na kuwa taifa moja lenye soko la pamoja, tungeweza kurahisisha biashara, kuongeza uzalishaji, na kuinua uchumi wa wananchi wetu," alisisitiza Hasunga.


Mbunge huyo aliongeza kuwa upatikanaji wa nishati safi ni suala la lazima katika maendeleo ya Afrika, akitolea mfano juhudi za Rais Samia katika kuhakikisha Watanzania wanapata nishati ya gharama nafuu. "Kama Afrika itaiga mfano wa Rais Samia katika kusimamia upatikanaji wa nishati safi, tutapunguza umasikini kwa kiwango kikubwa," aliongeza Hasunga.


Alieleza kuwa matumizi ya umeme wa uhakika na nishati safi kwa kupikia yatawasaidia wananchi kuokoa gharama, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, na kuimarisha sekta ya viwanda. Hasunga pia alizungumzia miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na serikali ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Reli ya Kisasa (SGR) inayotumia umeme unaozalishwa ndani ya nchi, akisema kuwa ni hatua kubwa katika mapinduzi ya miundombinu Afrika Mashariki.


Mbunge huyo alieleza imani yake kubwa kwa uzalendo wa Rais Samia, akisema kuwa kutokana na utendaji wake bora, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM walikubaliana kwa kauli moja kuwa anapaswa kuendelea kuongoza kwa miaka mingine mitano. "Rais wetu ana dhamira ya kweli ya kuendeleza nchi, na kazi yake imeleta mabadiliko makubwa kwa Watanzania. Kuanzia sekta ya elimu, afya, miundombinu, hadi uchumi wa nishati, yote inaonyesha mwelekeo mzuri," alisema Hasunga.


Aliwahimiza Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika juhudi zake za kuleta maendeleo, akisema kuwa kupitia ushirikiano wa kimataifa na mshikamano wa bara la Afrika, ndoto ya kuwa na bara lenye uchumi imara inaweza kutimia. Hasunga aliongeza kuwa umoja wa Afrika utawezesha bara hili kuwa na sauti moja katika masuala ya kimataifa, na kuimarisha nafasi yake katika medani ya siasa na uchumi duniani.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.