Wakati Watanzania wakielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mjadala kuhusu kuhalalisha kilimo cha bangi kwa ajili ya biashara umeingia kwa kasi kwenye majukwaa ya kisiasa. Hoja hii, inayotajwa kama suluhisho la ajira kwa vijana, imezua swali zito: Je, ni fursa ya kiuchumi au mtego utakaotumbukiza kizazi kijacho kwenye janga la uraibu na kupoteza dira?
Kisheria, msimamo wa Tanzania uko wazi. Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya Mwaka 2015 inaweka bangi kwenye kundi la dawa haramu. Matumizi yake yanaruhusiwa tu kwa shughuli za kitabibu au utafiti maalum chini ya kibali rasmi. Hii inamaanisha kuwa wanasiasa wanaojadili uhalalishaji wa kibiashara wanapendekeza sera inayokinzana moja kwa moja na sheria za nchi.
Wachambuzi wanaona hoja hii kama chambo rahisi cha kisiasa, kinacholenga kuvutia kura za vijana wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira, bila kuangalia madhara yake ya muda mrefu. Kuona bangi kama suluhisho la ajira ni sawa na kujaribu kuzima moto kwa kutumia petroli, kwani gharama za kiafya, kijamii, na kiusalama zinaweza kuwa kubwa kuliko faida za kiuchumi zinazotajwa.
Uzoefu wa kimataifa unatoa onyo kali. Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa takriban watu milioni 228 duniani walitumia bangi mwaka 2022. Nchini Canada, ambako ilihalalishwa mwaka 2018, matumizi miongoni mwa vijana yameongezeka kwa kasi, jambo ambalo wataalamu wa afya wanasema linaathiri ukuaji wa ubongo na kuleta madhara ya kudumu.
Hapa nchini, tayari vita dhidi ya bangi ni kubwa. Ripoti ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa zaidi ya tani 2,300 za bangi zilikamatwa, zikihusisha maelfu ya watuhumiwa. Takwimu hizi zinathibitisha kuwa tayari Tanzania ina tatizo kubwa la uzalishaji na usambazaji haramu; kuhalalisha kunaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi.
Hivyo, uchaguzi wa mwaka huu unawapa Watanzania jukumu la kihistoria. Ni fursa ya kuamua iwapo wanataka viongozi wenye sera endelevu za kujenga nguvu kazi yenye afya, ubunifu, na maadili, au watashawishiwa na ahadi za muda mfupi zenye uwezo wa kuharibu mustakabali wa taifa. Taifa lenye maendeleo ya kweli haliwezi kujengwa juu ya kizazi kilichodhoofishwa na uraibu.