Katika kile kinachoonekana kama mwendelezo wa vita baridi ya kiteknolojia kati ya mataifa makubwa duniani, Marekani imetoa onyo jipya linaloashiria kuwa China haitegemei 'silaha' moja tu katika ulimwengu wa Akili Mnemba (Artificial Intelligence). Kama ilivyo desturi ya mchezo wa bao, ukiziba hapa, mwenzako anapita kule; ndivyo hali ilivyo sasa baada ya serikali ya Washington kuitaja kampuni ya Moonshot AI kama tishio jipya na mchezaji muhimu katika kizazi kipya cha mifumo ya AI iliyo wazi (open models).
Ripoti mpya kutoka Kituo cha Viwango na Ubunifu wa AI (CAISI), ambacho kiko chini ya Wizara ya Biashara ya Marekani, imebainisha wazi kuwa utawala wa China katika sekta hii haujakomea kwenye kampuni ya DeepSeek pekee ambayo ilitikisa dunia hivi karibuni. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa makampuni ya Kichina yanayotengeneza mifumo ya kisasa ya 'open-weight' yanaongezeka kama uyoga wakati wa mvua, jambo linaloipa Marekani tumbo joto.
Ripoti ya Pili Chini ya 'Mpango wa Trump'
Hii ni ripoti ya pili kutolewa kufuatia agizo la Rais Donald Trump kupitia 'Mpango Kazi wa AI' (AI Action Plan) alioutangaza mwezi Julai. Lengo kuu la mpango huu ni kuchunguza kwa kina uwezo, utendaji, na viwango vya udhibiti (censorship) wa mifumo ya kisasa ya AI kutoka China. Ikumbukwe kuwa ripoti ya kwanza iliyotoka Septemba ilionyesha wasiwasi mkubwa kuwa DeepSeek inaweza kuwa hatari kwa usalama wa taifa wa Marekani. Sasa, jicho la mwewe limehamia kwa Moonshot AI.
Kimi K2 Thinking: "Kijana" Mpya Mtaani
Mjadala mkuu katika ripoti hii unamhusu 'mtoto' mpya wa Moonshot AI anayeitwa ‘Kimi K2 Thinking’. Mfumo huu ulizinduliwa Novemba mwaka jana na uliacha gumzo kubwa kwenye jumuiya ya kimataifa ya TEHAMA kutokana na uwezo wake wa kuandika makala na uchambuzi kwa ufasaha wa hali ya juu. Wataalamu wanaufananisha mfumo huu na ule mshtuko wa "DeepSeek Moment" kwa sababu ya ufanisi wake mkubwa huku ukigharimu fedha kidogo kuendesha.
Hata hivyo, CAISI imekiri kuwa licha ya sifa hizo, Kimi K2 bado haijafikia kiwango cha matumizi makubwa kama ilivyo kwa DeepSeek au mifumo ya OpenAI (kama gpt-oss), wakitumia takwimu za kupakuliwa kutoka mtandao wa Hugging Face kama kigezo.
Kwenye upande wa utendaji wa kiufundi, ripoti hiyo inadai kuwa Kimi K2 bado inasuasua ikilinganishwa na vigogo wa Marekani kama ‘GPT-5’ ya OpenAI au ‘Opus 4’ ya Anthropic, hasa katika masuala ya uhandisi wa programu (software engineering) na kazi za mtandaoni zinazohitaji utatuzi wa changamoto ngumu za kiusalama (cyber tasks).
Siasa za Lugha na Udhibiti wa Maudhui
Jambo la kushangaza na la kuvutia zaidi katika ripoti hii ni jinsi mfumo huu unavyofanya kazi kwa ndimi mbili. CAISI walitumia kipimo chao maalum kiitwacho ‘CCP-Narrative-Bench’ kupima jinsi Kimi K2 inavyojibu maswali nyeti ya kisiasa.
Matokeo yalionyesha "undumilakuwili" wa kiteknolojia: Mfumo huo unadhibitiwa vikali sana unapotumia lugha ya Kichina, ukifuata sera kali za ndani za China. Lakini unapotumia lugha za kigeni kama Kiingereza, Kihispania, au Kiarabu, udhibiti huo unalegezwa kiasi. Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kupima udhibiti huo hadi kwenye lugha za Kiarabu na Kihispania, ikionyesha jinsi China inavyolenga soko la kimataifa. Hali hii inafanana na ile ya mfumo wa ‘Qwen3-Next’ wa Alibaba Cloud.